Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliwasihi wananchi kufanya mazoezi ili kuimarisha afya ya mwili hivyo kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. Chalamila aliyasema hayo alipozindua maandalizi ya CRDB Bank Marathon inayotarajiwa kufanyika Agosti 13 jijini Dar es Salaam ikiwashirikisha wakibiaji 7,000 kutoka kila pembe ya dunia.
“Mlio hapa naamini kabisa mnafahamu umuhimu wa mazoezi kwa afya zetu hasa katika kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. Mimi binafsi nawasihi wana Dar es Salaam kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zetu. Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa akituasa sana juu ya umuhimu wa kufanya mazoezi. Nimefurahi leo kuwa hapa kwani nimepata wasaa wa kuchangamsha damu kidogo,” amesema Chalamila.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kwa muda mrefu amekuwa akizisikia mbio za CRDB Bank Marathon na baada ya kuja mjini sasa amepata nafasi ya kushiriki maandalizi ya msimu wa nne wa mbio hizo za hisani za kimataifa.
Zilipoanzishwa mwaka 2019, mbio hizo zilikusudia kufanikisha matibabu ya watoto 100 wenye matatizo ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na mwaka uliofuata fedha zilizopatikana zikijenga kituo cha huduma katika Taasisi ya Saratani Ocean Road kabla mwaka jana hazijawanufaisha wanawake wenye fistula na ujauzito hatarishi katika Hospitali ya CCBRT.
Kwenye mbio za mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema watafanikisha matibabu ya upasuaji wa moyo kwa Watoto, matibabu ya wanawake wenye ujauzito hatarishi na wale wenye fistula pamoja na kujenga kituo cha afya visiwani Zanzibar.
“Haya ni makundi muhimu katika jamii yetu na wana uhitaji wa kuwa na afya njema, ni nguvukazi ya kutosha kushiriki ujenzi wa Taifa letu. Fedha zote zinazopatikana kutoka kwa washiriki wa CRDB Bank Marathon zitatumiwa kwa malengo haya yaliyotajwa hivyo kila mshiriki anachangia upatikanaji wa huduma bora za afya.
“Nawasihi Watanzania wenzangu hasa kutoka Dar es Salaam na nchi nzima kwa ujumla kujisajili ili kushiriki mbio hizi huku kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaweka tofauti katika jamii na kuacha alama chanya,” amesema Nsekela.
Kujiandikisha kwenye mbio hizi zitakazoishirikisha familia nzima zikiruhusu wakimbiaji wa kilomita tano, 10, 21 na 42, kwa mtu mmoja ni Sh45,000 tu lakini kwa kikundi chakuanzia watu 30 ni Sh40,000 kila mmoja.