Home BUSINESS BENKI YA CRDB YATUNUKUWA TUZO YA KIMATAIFA YA UBORA NA TAASISI ...

BENKI YA CRDB YATUNUKUWA TUZO YA KIMATAIFA YA UBORA NA TAASISI UMOJA WA ULAYA

 
Benki ya CRDB kwa mara nyingine imetunukiwa tuzo ya kimataifa ya ubora na Taasisi ya Umoja wa Ulaya ijulikanayo kama ESQR (European Society for Quality Research).  Tuzo hiyo imetolewa Jumapili, t Julai 9, 2023 jijini Brussels Ubeligiji, yalipo makao makuu ya Umoja wa Ulaya ambao hivi karibuni umetoa ufadhili wa Euro Milioni 179.35 kwa Serikali ya Tanzania kusaidia mabadiliko ya sera, ukuaji wa viwanda na maendeleo ya miuondombinu.
 
Taasisi ya ESQR inajulikana kutokana na juhudi zake za kuhamasisha uvumbuzi na ubora katika sekta mbalimbali duniani. Tuzo hii ni kielelezo cha jitihada za Benki ya CRDB katika kutoa huduma bora za fedha pamoja na mchango wake mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na maendeleo kwa ujumla.
 
“Tunajisikia faraja na heshima kubwa kupokea tuzo hii kutoka kwa ESQR (European Society for Quality Research),” alisema Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB. Tuzo hii kubwa ni kielelezo tosha cha juhudi na kujitoa kwa wafanyakazi wetu ambao siku zote wana dhamira ya kuhakikisha wanatoa huduma za kipekee kwa wateja wetu. Tunapoendelea kutelekeleza mkakati wetu wa biashara wa muda wa kati, tumejidhatiti kuhakikisha tunaendelea kusimamia ubora na uvumbuzi katika kila tunachokifanya ili tuweze kuwa vinara katika masoko yote tunayoyahudumia.
Kupatikana kwa tuzo hii ya ubora kwa Benki ya CRDB ni hatua muhimu katika safari ya benki kuhakikisha inakua kinara wa ubora katika utoaji wa huduma za fedha, Lakini pia tuzo hii inaendelea kuiweka Benki ya CRDB katika nafasi bora ya kuwa taasisi ya fedha inayoaminika ambapo mnamo mwezi Machi 2023, Benki ilipokea kiasi cha Euro Milioni 150 kutoka kwa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (European Investment Bank) kwa ajili ya kusaidia biashara changa, ndogo na za kati nchini Tanzania.
 
Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji, Mheshimiwa Jestas Nyamanga, alihudhuria hafla ya kukabidhiwa tuzo ya ubora kwa Benki ya CRDB na kuonyesha furaha yake kwa Benki ya Tanzania kutunukiwa tuzo kubwa ya kimataifa ambapo alinukuliwa akisema, “Tunajivunia tuzo hii ya Benki ya CRDB kutoka kwa taasisi hii kubwa ya Ulaya. Tuzo hii inadhihirisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi ili iweze kufanya vizuri.”
Kwa upande wake, Mshauri Mtendaji Mkuu wa ESQR, Bw. Michael Harris ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuchukua tuzo hiyo ya ubora kwa mara ya pili baada ya kutunukiwa tena tuzo hiyo mwaka 2021. ” Naitakia Benki ya CRDB mafanikio zaidi ili iweze kuendelea kuleta utofauti katika masoko inayohudumia lakini zaidi iendelee kuongoza masoko hayo wa uadilifu, uwazi lakini kubwa zaidi ubinadamu kwa kugusa maisha ya watu inayowahudumia,” alisema Michael.
 
Tangu Januari 2023, Benki ya CRDB imetunukiwa tuzo zaidi ya 13 ikiwemo tuzo ya Benki Bora Tanzania inayotolewa na Global Finance Magazine, Benki Bora Tanzania kwa kuhudumia biashara ndogo na za kati inayotolewa na Global Finance pamoja na Benki Bora ya Kanda inayotolewa na African Banker. Benki inaendelea na jitihada zake za kuchangia ukuaji wa uchumi na kuwezesha watu binafsi na biashara kufanikiwa. Vile vile, Benki itaendelea kujikita katika kutatua mahitaji ya wateja kwa kutoa huduma za kibunifu zinazokidhi mahitaji ya wateja yanayobadilika kila uchao pamoja na jamii inazozihudumia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here