Na Maiko Luoga Mpanda.
Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa amewashauri viongozi wa dini nchini wakiwemo Maaskofu na Makasisi, kutojiingiza kwenye mijadala inayoendelea kwenye majukwaa mbalimbali yakihusisha wanasiasa na wataalamu wa sheria.
Askofu Mndolwa alitoa ushauri huo julai 30 mwaka huu kwenye Ibada ya kumweka wakfu Askofu wa pili wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Lake Rukwa Ephraim Ntikabuze iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Dayosisi hiyo Kristo Mfalme Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Alisema kwasasa kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya mkataba wa Bandari ambao kwa asilimia kubwa umeteka hisia za watu tofauti nchini na kusababisha baadhi ya viongozi wa dini kuingia kwenye majukwaa ya kisiasa na kushiriki malumbano na wanasiasa pamoja na wanasheria.
Aliongeza kuwa viongozi wa Dini kote nchini wanayo nafasi maalumu ya kuwaita viongozi wa Serikali na kuwashauri mambo tofauti yanayolalamikiwa na wananchi ambao ni waumini wa Makanisa na misikiti ili yaweze kupata ufumbuzi badala ya kushiriki mijadala hiyo kupitia majukwaa ya kisiasa.
“Sisi hatukatazi watu kujadili maendeleo ya Taifa lakini tunaona kuna hatari, baadhi ya viongozi wa dini na Kanisa wameanza kuingia kwenye majukwaa mbalimbali na kushiriki malumbano na wanasiasa pamoja na wanasheria jambo ambalo ni kinyume na maadili ya dini.”
“Serikali kupitia Mhe, Rais hawajazuia nafasi ya kushauriana na viongozi wa dini si jambo jema sisi kusimama kwa nafasi yetu na kuingia kupambana kwenye majukwaa hayo, Rais na viongozi wote wa Serikali ni waumini wetu makanisani na misikitini tungeweza kuwaita na kuwasikiliza maoni yao na sisi tukashauri tunachokiona”
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalumu) Mhe, George Mkuchika alisema hivi karibuni Bunge la Tanzania liliridhia mkataba au makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu kuendeleza Bandari ya Dar es Salaam.
“Hii haitakuwa mara ya kwanza kukaribisha mwekezaji, kwa miaka 22 kulikuwa na Kampuni iliyoendesha baadhi ya shughuli katika Bandari ya Dar es Salaam hadi Serikali tuliposema sasa basi ili tutafute mtu mwenye uwezo zaidi” Alisema Mhe, George Mkuchika.
Akizungumza mara baada ya kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa pili wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Lake Rukwa Ephraim Ntikabuze aliahidi kushirikiana na Taasisi mbalimbali za dini katika mikoa ya Rukwa na Katavi huku akiwaomba waumini kuimarisha umoja uliopo katika Dayosisi hiyo.
Ephraim Ntikabuze amewekwa wakfu kuwa Askofu wa pili wa Dayosisi ya Lake Rukwa baada ya aliyekuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi hiyo Mathayo Kasagara kumaliza muda wake wa utumishi ndani ya Kanisa hapo machi 26, 2023.