Na: Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu mwaka hadi mwaka ili kuongeza wigo wa wanufaika.
Kauli hiyo imetolewa bungeni Dodoma leo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara aliyeuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kuhakikisha wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha sita wanapata mikopo ya Elimu ya Juu.
“Bajeti ya Mikopo iliongezeka kutoka Shilingi bilioni 570 mwaka 2021/2022 hadi Shilingi bilioni 654 mwaka 2022/2023. Pia, Mwaka 2022/2023 Shilingi bilioni 3 zilitengwa kwa ajili ya Samia Scholarship iliyonufaisha wanafunzi 593 waliohitimu kidato cha sita wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM)”. Alisema Naibu Waziri Kipanga.
Alifafanua kuwa katika kuendelea kupanua fursa za mikopo kwa wahitimu wa kidato cha sita, Serikali imeingia mkataba wa mahusiano na Benki ya NMB ili kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 9 kwa wazazi au walezi kwa ajili ya kugharamia elimu ya watoto wao katika ngazi ya Elimu ya Juu na Kati.
“Aidha, Serikali itaendelea kutafuta fursa za Mikopo ya Elimu ya Juu kutoka kwa Wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila mhitimu wa kidato cha sita mwenye sifa anapata mkopo kwa ajili ya kugharamia Elimu ya Juu”. Alimaliza Naibu Waziri Kipanga.