Home BUSINESS WACHIMBAJI MADINI KUJIFUNZA KEKNOLOJIA MPYA CHINA

WACHIMBAJI MADINI KUJIFUNZA KEKNOLOJIA MPYA CHINA

Na: Beatrice Sanga -MAELEZO

JUMLA ya Wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa madini nchini 260 wanatarajia kwenda nchini China Julai mwaka huu kwa ajili ya kujifunza Teknolojia zitakazowasaidia kupata masoko ya kimataifa.

Wachimbaji hao wamesema wameweka mkakati wa kubaini masoko ya kimataifa yenye uwezo kuhakikisha sekta hiyo inakuwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam June 22, 2023 Kamishna Msaidizi wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Maruvuko Msechu amesema serikali ina makakati wa kufungua masoko ya kisekta ya madini ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na maendeleo.

“Sekta ya madini ni muhimu katika uchumi kwani huongeza ajira, kupunguza umaskini na kuleta maendeleo ya kijamii, lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa masoko, ufadhili wa kutosha, na maendeleo madogo ya kiteknolojia,” ameeleza Msechu.

Alisema mikakati iliyoweka na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itasaidia kufungua masoko ya kimataifa ya madini ili kujenga fursa na kuongeza wawekezaji.

“Serikali imeweka mikakati ya kubaini masoko ya kimataifa yenye uwezo kuhakikisha sekta hiyo inakuwa, pia kujengeana uwezo kuimarisha ushindani kwa wachimbaji wadogo, mikakati hiyo inalenga kufungua uwezo wa sekta na kuandaa fursa kwa wachimbaji wa madini wafanyabiashara na wawekezaji,” ameeleza Msechu.

Msechu amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na utafiti wa masoko, kujengeana uwezo kwaajili ya kuimarisha uzalishaji na uchimbaji wa madini kwa ufanisi zaidi, maendeleo ya miundombinu, na matumizi ya Teknolojia za kisasa katika sekta ya madini na watahakikisha wanawawezesha wachimbaji Madini hususani wadogo kuyafikia masoko ya kimataifa ya ndani na nje ya nchi kwa kuwezesha kuwepo na mifumo ya haki na uwazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) , Dkt.Venance Mwese alisema wanao mkakati wa kuanzisha benki ya wachimbaji nchini hivyo aliwataka kwenda kupata teknolojia halisi itakayosaidia upatikanaji wa masoko.

“Mjipange kwani hii fursa ni ya kitaifa hivyo atakayetafuta mwekezaji ahakikishe ameenda akiwa amejipanga na mwisho wa ziara hiyo natarajia mtabadilishana mikataba na kupeana mawasiliano,” ameeleza Dkt. Mwesse.

Naye Mwenyekiti wa Touch Road International Group Dr. He I LIEHUI amesema kuwa wana nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa sekta ya madini nchini inaongeza ufanisi kupitia elimu na ujuzi ambao watashirikiana nao hususani katika wakati huu ambapo mabadiliko ya teknolojia ni makubwa lakini pia kuwaeleza juu ya sheria na kanuni wanazozitumia katika kusafirisha na kuaigiza teknolojia hizo.

“Tutawaonesha wachimba madini machine zipi za muhimu katika sekta ya uchimbaji madini Tanzania ili kwamba wanaweza kuziagiza na kuzitumia katika shughuli za uchimbaji madini, lakini pia teknolojia ni jambo muhimu sana hivyo tutajadiliana na wachimbaji madini wa Tanzania ili kufahamu teknolojia kubwa za kisasa na namna zinavyofanya kazi, hivyo hatuna budi kuwaonesha watanzania na wao wazijue ili kuendana sambamba na uchimbaji madini kama unavyofanywa na kampuni za kichina.” Amesema Bw. He I LIEHUI.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Shirikisho la Wachimbaji Wadogo nchini (FEMATA), Alfred Luvanda alisema wafanyabiashara hao na wachimbaji wataondoka Julai 20, mwaka huu kwenda China na watakuwa na ziara ya siku 10 na kurejea nchini Julai 30, mwaka huu.

“Tutakutanishwa na kujadiliana na watoa huduma za fedha yaani benki, tutakutanishwa na tutajadiliana na wazalisha mitambo ya uchimbaji na usafirishaji madini, tutatembelea viwanda mbalimbali na kujadili fursa za kukuza teknolojia, tutapata fursa ya kuonesha bidhaa zetu na kuwa na siku ya maonesho na kuuza bidhaa tutakazokwenda nazo, lakini pia tutapata fursa ya kuwaalika na kujadili mikataba ya ushirikiano,” amefafanua Luvanda.

FEMATA wameeleza kuwa mpaka sasa wafanyabiashara, wachimbaji na wadau wa madini 260 wanatarajia kusafiri kuelekea China katika awamu ya kwanza na 100 tayari wameonesha nia ya kusafiri na gharama za safari ni dola 370 na wanatarajiwa kutembelea majimbo tisa nchini China.

Wachimbaji hao baada ya kukamilisha ziara yao wanatarajiwa kurudi na kundi la watalii zaidi ya 200 ambao watafika Tanzania kupitia ndege ya Shirika la Ndege nchini (ATCL).

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here