Home LOCAL MATUMIZI HOLELA YA DAWA YANAWEZA KUSABABISHA USUGU WA DAWA – DKT. CHIWANGA

MATUMIZI HOLELA YA DAWA YANAWEZA KUSABABISHA USUGU WA DAWA – DKT. CHIWANGA

Jamii imeshauriwa kuacha matumizi holela ya dawa kwa kuwa matumizi hayo yanaweza kusababisha usugu wa dawa au kupata madhara ya kiafya na kwamba ni vema jamii ikazingatia maelekezo na ushauri wa Wafamasia.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila Dkt. Faraja Chiwanga kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH wakati wa kuhitimisha wiki ya famasi iliyofanyika Juni 10 hadi 16 iliyoongozwa na kauli mbiu ‘famasi ni nguzo ya mfumo wa afya uliothabiti, imara na bora’

Dkt. Chiwanga ameongeza kuwa uongozi umefurahishwa na kitendo cha wafamasia kutoa elimu kuhusu matumizi na uhifadhi sahihi wa dawa hususani kwa wanafunzi, wagonjwa na ndugu wa wangonjwa kwakuwa dawa ikitumika isivyotakiwa inaweza kusababisha madhara makubwa.

“Wiki ya famasi iendelee kuwa chachu kwenu ya kuikumbusha jamii na muendelee kufanya kazi kwa bidii, nidhamu, weledi na uaminifu ili kulinda heshima ya taaluma yenu kwakuwa mtu mmoja akiharibu inaitia doa taaluma nzima” ameongeza Dkt. Chiwanga.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Famasi MNH-Mloganzila Bw. Dominic Mfoi ameeleza kuwa kwa mwaka huu wiki ya famasi imeadhimishwa kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuendesha zoezi la uchangiaji damu ambapo wamefanikiwa kukusanya uniti 61 kati 30 walizolenga kukusanya.

Pia wametoa elimu kwa wanafunzi 305 wa Shule ya Msingi na Sekondari ya Mloganzila kuhusu matumizi sahahi ya dawa na madhara yake endapo zitatumika kwa kutofuata ushauri wa mfamasia.

Wiki ya Famasi hufanyika Juni 10-16 kila mwaka ambapo wafamasia wa Jumuiya ya Madola huonesha shughuli wanazozifanya na kutafakari mustakabali wa taaluma yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here