Home Uncategorized CHUO CHA UTALII KUWANOA WAFANYAKAZI WA MUHIMBILI KWENYE UKARIMU

CHUO CHA UTALII KUWANOA WAFANYAKAZI WA MUHIMBILI KWENYE UKARIMU

Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kitaingia kwenye makubaliano na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) yenye lengo la kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wote wa hospitali kwenye masuala ya ukarimu (hospitality) na namna ya kutoa kiwango cha juu cha huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi wakati wa mazungumzo kati yake na Afisa Mtendaji Mkuu wa NCT, Dkt. Florian Mtey alipotembelea MNH kuona namna ambavyo taasisi hizo zinaweza kushirikiana katika maeneo mbalimbali.

Prof. Janabi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kuratibu Utalii Tiba nchini, amesema, Serikali ya awamu ya sita imewekeza sana kwenye sekta ya afya kuanzia ngazi ya Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, Mkoa, Kanda hadi Taifa lakini bado kuna changamoto ya ukarimu wakati wa kuhudumia wananchi.

“Ni kweli kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na changamoto ya kukosekana ukarimu wakati wa kutoa huduma za matibabu na bado tuko nyuma kama baadhi ya nchi nyingine zinazoendelea Kusini mwa Jangwa la Sahara kama watoa huduma. Tunaweza kufanya upasuaji mzuri, tukapandikiza figo, uloto……lakini ile huduma bora kwa mteja tunahitaji kuiboresha. Sisi kwetu kama MNH ni jambo lenye afya na bora, hivyo tutashirikiana na NCT kuliboresha ili tuwe na watu wanaoweza kutoa huduma za ziada wanapomhudumia mwananchi, hapo ndio tutaweza kutoa huduma bora na si bora huduma”, amesisitiza Prof. Janabi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa NCT, Dkt. Florian Mtey ameipongeza MNH kwa kazi kubwa ya kuhudumia wananchi wa ndani na nje na kuongeza kuwa kuna mabadiliko makubwa sana ya kiutendaji tangu Prof. Janabi ateuliwe kuisimamia MNH.

Dkt. Mtey amesema NCT imeona fursa kubwa ya kushirikiana na MNH katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuleta wanafunzi wake kupata mafunzo kwa njia ya vitendo (intership) katika maeneo wanayofundisha ikiwemo, mapokezi, ukarimu na masuala ya kuhudumiwa wateja.

“Kwa kuanza mashirikiano haya tutaanza kwenye maeneo ya utoaji mafunzo kwa watumishi wote wa MNH hasa kwenye ukarimu na huduma bora kwani sisi tuna weledi na ubobezi kwenye maeneo hayo na pia wanafunzi wetu katika maeneo hayohayo watanufaika na mafunzo kwa njia ya vitendo, amesema Dkt. Mtey.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here