Home BUSINESS TANZANIA MLANGO WA AFRIKA KATIKA FURSA ZA UWEKEZAJI MADINI

TANZANIA MLANGO WA AFRIKA KATIKA FURSA ZA UWEKEZAJI MADINI

Na: Beatrice sanga MAELEZO

Tanzania imekuwa ni kivutio cha shughuli za uchimbaji na biashara ya madini Barani Afrika na nchi nyingine nje ya Afrika kutokana na kupiga hatua katika sekta hiyo muhimu katika uchumi wa Nchi kupitia fursa za uwekezaji wa madini mkakati na muhimu

Hayo yameelezwa Mei 23, 2023 na waziri wa madini nchini Dkt. Doto Biteko katika uzinduzi rasmi wa kongamano la uwezeshaji katika sekta ya Madini mwaka 2023 linalojulikana kama Tanzania Mining & Investment Forum 2023, ambalo linatarajiwa kufanyika Oktoba 25-26 mwaka huu na linatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 2000 kutoka Tanzania na Nje ya Tanzania ambapo litaelezea fursa mbalimbali ambazo zinapatikana hapa nchini katika sekta ya madini.

Dkt, Biteko amesema kuwa mkutano huo ambao tangu mwaka 2020 umekuwa ukifanyika mwezi wa Pili tarehe 22, kila mwaka lakini mwaka huu wizara imeamua kubadilisha tarehe ya kufanya mkutano huo.

“Tumefanya kwa miaka yote kwa mfululizo isipokuwa mwaka huu, tumeamua kubadilisha tarehe kwasababu mwezi wa pili kuna mikutano mingine mingi ya kimataifa inafanyika kwenye mataifa mengine, kwahiyo tulivyoangalia kalenda ya mikutano yote ya madini duniani tukaona nafasi iko mwezi wa kumi na baada ya kushauriana na waratibu tumeona tufanye mkutano mwezi huo, lengo la mkutano huu ni pamoja na kuwasilisha taarifa muhimu za Sekta za Madini, kuimarisha ushirikiano wa vikao vya mazungumzo na wawekezaji, kubainisha fursa zilizopo kwenye miradi na kuimarisha ushirikiano wa ndani na nje ya nchi katika kukuza sekta ya madini na kuifanya sekta ya madini Tanzania kuwa endelevu.” Amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amesema kuwa mkutano wa mwaka huu utafanyika kwa kuwakutanisha washiriki kutoka sehemu mbalimbali duniani ambao utaleta tija zaidi katika Sekta ya Madini nchini.

“Toka mwezi wa pili mwaka huu tumekuwa na mikutano midogo midogo ya sekta ya madini kwenye makundi yao, wachimbaji wa madini tumekuwa na mkutano nao pekee yao, wafanyabiashara wa madini tumekuwa na mkutano wao pekee yao, wachimbaji wa madini ya viwandani tumekuwa na mkutano nao pekee yao na makundi mengine ya madini kwasababu hasara tuliyokuwa tunaipata kwenye mikutano hii ya madini kundi moja la madini linameza makundi mengine.” Ameeleza Dkt. Biteko.

Biteko amesema kuwa mkutano huo utaleta wageni ambao pia watashiriki kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini, “Tunataka kufungamisha sekta ya madini na sekta ya utalii, wale wataokuja kwaajili ya mkutano huu, wengine wameshakata tiketi kwaajili ya kwenda kutembelea mbuga zetu za wanyama, wengine wamekata tiketi kwenda kutembelea Zanzibar ni kwasababu ya uwepo wa mkutano huu.” Amesisitiza Dkt. Biteko.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ocean Business Patners Tanzania Ltd Abdulsamad Abdulrahim amesema kuwa wazawa wana nafasi kubwa ya kutumia fursa zilizopo nchini katika sekta ya madini ili kuwanufaisha wao na uchumi wa nchi kwa ujumla hivyo amewaomba watanzania kuendelea kuwekeza katika sekta ya madini.

“Katika mkutano huu, kutakuwa na maonesho ambayo yataonesha bidhaa zote za madini zilizopo hapa Tanzania, vilevile tumejipanga kuleta nchi ambazo zimepiga hatua na zimekuwa mfano mzuri wa mataifa yao na nchi ambazo zimesaidia raia wao kukua, lakini vile vile tutawaleta wabobezi waliobobea katika sekta hii ambao wataizungumzia hii sekta.” Amesema Abdulrahim

Serikali imeweka sheria na kanuni za kuwezesha njia bora za uchimbaji wa madini kwaajili ya usalama wa jamii na mazingira zinazoshabiana na za kimataifa, lakini pia imeweka kipaumbele katika suala la uongezaji thamani na uchakati wa madini nchini ili kuongeza ajira, mapato na pia kuimarisha biashara miongoni mwa watanzania, lakini pia Tanzania ni mwanachama wa taasisi ya uhamasishaji uwazi na uwajibikaji (Extractive Industries Transparency initiative-TEITI) katika rasilimali madini mafuta na gesi asilia inayozingatia uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa madini na maliasili kwa ujumla.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here