Idadi ya Wahitimu katika Mahafali ya katikati ya mwaka kwa masomo (Mid-year Graduation) katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA imeongezeka kutoka Wahitimu 209 kwa mwaka 2022 hadi 274 kwa mwaka 2023 ambapo kati ya hao watunukiwa wanawake ni 91 sawa na asilimia 33.2 ya wahitimu wote.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda ameyasema hayo kwenye Mahafali ya 41 ya Katikati ya mwaka yaliyofanyika Kampasi Kuu ya Edward Moringe na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Chuo hicho Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.
Prof. Chibunda amesema kuwa wanastahili kujipongeza kwa mafanikio ambayo wameendelea kuyapata kila mwaka ya kuongeza idadi ya nguvu kazi na yenye Taaluma stahiki nchini ambapo mafanikio hayo yanatokana na ufanyaji kazi mzuri wa Viongozi wa chuo, Waadhiri na wafanyakazi wote wa chuo hicho ambao umewawezesha kupiga hatua zaidi mwaka hadi mwaka.
‘‘Mahafali ni tukio la kipekee sana kokote pale duniani, kwa wahitimu tukio hili ni muda mahususi kwa kusheherekea na kutathmini miaka kadhaa waliotumia katika kuhakikisha wanafikia malengo yao”. Alisema Prof. Chibunda
Ameongeza kuwa Chuo kimeendelea kutekeleza malengo na majukumu yake kupitia katika ndaki zao zote saba (7), Shule kuu ya Elimu, Kurugenzi na Taasisi zake tangu Mahafali ya 40 Novemba 2022 ikiwemo utekelezaji wa shughuli za mafunzo ambazo zimeendelea kufanyika chuoni hapo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo( SUA) Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, amesema Takribani miezi sita tangu kufanyika kwa Mahafali ya 40 katika kipindi hicho Baraza limetekeleza majukumu yake makuu kwa ufanisi mkubwa ikiwemo kusimamia Menejimenti ya Chuo ili itemize majukumu ya chuo ambayo ni kutoa Mafunzo, kufanya Tafiti, kutoa Huduma za Kitaalam na Ugani vilevile kuzalisha Mali.
Mwisho.