Home LOCAL SERIKALI YATOA BILIONI 99.3 KUTEKELEZA MIRADI YA KIMAENDELO MKOA WA GEITA

SERIKALI YATOA BILIONI 99.3 KUTEKELEZA MIRADI YA KIMAENDELO MKOA WA GEITA

Na: Costantine James, Geita.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema kuwa Serikali itaendelea kusogeza ipasavyo huduma za msingi kwa wananchi katika sekta ya Afya, Elimu, Maji na Miundombinu ya Barabara ili kuleta maendeleo chanya kwa wananchi.

Chongolo ameyasema hayo leo Mei 15, 2023 katika hafla ya uzinduzi wa Ukumbi wa mikutano wa CCM na uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa nyumba ya kupumzikia viongozi (Rest House) katika wilaya ya Bukombe Mkoani Geita.

Akizungumza na wanachama wa CCM, viongozi wa Serikali na Wananchi Ndugu Chongolo amewapongeza viongozi wa Chama hicho kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya na kwamba serikali ya awamu ya sita itaendelea kuboresha huduma za msingi kwa Wananchi.

Chongolo amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya bilioni 99.3 kwa mkoa wa Geita kwa lengo la kuendeleza kutekeleza miundombinu mbalimbali ya kimaendeleo kwa lengo la kusogeza huduma za msingi kwa Wananchi katika sekta ya Afya, Elimu, maji na miundombinu ya Barabara.

Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri wa madini Dkt Dotto Biteko amesema ushirikiano baina ya viongozi wa Serikali na Chama katika wilaya ya Bukombe na Mkoa wa Geita kwa ujumla eneo ndio chachu ya maendeleo kwa wananchi.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa Ukumbi wa mikutano wa CCM na nyumba ya kupumzikia viongozi (Rest House) Mkuu wa wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita Said Nkumba amesema ujenzi humo umeghalimu zaidi ya milioni 200.

Nkumba amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri wa Madini Dkt Dotto Biteko kwa mchango wake mkubwa wa kuwezesha ujenzi huo kwani katika ujenzi huo amechangia zaidi ya asilimia 80 huku asilimia 20 zikichangiwa na wanachama wa Ccm wilaya na Mkoa wa Geta.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here