Home LOCAL RAIS SAMIA AMEREJESHA MATUMAINI YA WATANZANIA – NGOs

RAIS SAMIA AMEREJESHA MATUMAINI YA WATANZANIA – NGOs

* Wampongeza kwa uongozi wa kimageuzi.

Mwandishi Wetu

MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali nchini (NGOs) yamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wa kimageuzi tangu aliposhika madaraka miaka miwili iliyopita, yakisema kuwa Rais Samia amerejesha matumaini ya Watanzania kwenye uchumi, demokrasia na maendeleo ya jamii.

Umoja wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania (TANGO) umesema kuwa Rais Samia ameleta mageuzi makubwa katika nyanja za uchumi, huduma za jamii na demokrasia katika kipindi kifupi tangu alipoingia madarakani Machi 17, 2021.

“Bodi ya Wakurugenzi na Sekreterieti ya TANGO inapenda kimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Taznania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kufufua matumaini mapya ya Watanzania kwenye nyanja za uchumi, kijamii na kisiasa,” TANGO ilisema katika taarifa yake kwa umma.

“Tunampongeza Rais kwa falsafa yake ya kimageuzi aliyoibuni ya “4Rs” Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding of the Nation (Ujenzi Upya wa Taifa).”

TANGO imesema kuwa falsafa hiyo ya 4Rs ya Rais Samia ni msingi wa ukuaji wa uchumi na demokrasia ya vyama vingi.

Umoja huo wa NGOs umesema kuwa unatambua aina mpya ya utawala bora na uongozi ambao uletwa na Rais Samia kwenye Awamu ya 6, ambao umepanua uwanja wa uhuru wa wananchi mmoja mmoja na kwenye makundi kutoa maoni yao kwa lengo la kuleta maendeleo kwa taifa na watu wake.

TANGO imesema kuwa maamuzi ya Rais Samia kuongeza uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari na kuruhusu vyama vya upinzani vifanye mikutano ya hadhara ni ishara kuwa yeye ni muumini wa uongozi unaojenga umoja wa taifa kwa kusimamia katiba na sheria za nchi.

Kwa mujibu wa TANGO, mashirika yasiyo ya kiserikali yamenufaika na utawala wa Rais Samia kutokana na NGOs nchini kufanya kazi kwa uhuru zaidi bila ya kuingiliwa na Serikali, tofauti na miaka mitano iliyopita.

“Wizara za Serikali chini ya utawala wa Rais Samia zimekuwa na mahusiano ya kirafiki na NGOs, tofauti na miaka ya nyuma. Zaidi ya hapo, Rais ameagiza pia mamlaka ya mapato itatue changamoto za kikodi za NGOs,” ilisema taarifa hiyo.

“Dk. Samia pia alivifungulia vyombo vya habari kadhaa ambavyo vilifungiwa miaka ya nyuma,” taarifa hiyo ilisisitiza.

“Sisi kama TANGO tunaunga mkono juhudi za kimageuzi za Rais Samia zenye lengo la kuongeza kasi ya maendeleo ya Tanzania.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here