Na.Alex Sonna-SINGIDA
MKURUGENZI wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Professor Mwera Foundation,Hezbon Mwera ameitaka jamii kuwapeleka katika Vyuo vya Ufundi wanafunzi waliomaliza au wanaosubiria matokeo ya kidato cha nne na darasa la saba ili waweze kusomea kozi za muda mfupi ambazo zitawasaidia kuongeza utaalamu.
Pia, ameiomba serikali kuanzisha mfuko wa elimu katika kila Halmashauri lengo likiwa ni kusimamia ubora wa elimu.
Prof. Mwera ameyasema wakati akizungumza na walimu
hao kwenye mkutano wa wadau wa elimu mkoa wa Singida wa mwaka 2023 ambapo amesema kwa kusoma kozi za muda mfupi zitawaongezea sifa mbalimbali katika utendaji kazi wao katika miaka ya baadae.
Pia ameziomba Halmashauri kuanzisha mfuko wa elimu kwani utasaidia kuweka sawa ubora wa elimu pia kusaidia vijana wenye uhitaji ndani ya halmashauri zao.
Vilevile, amesema wazazi wana jukumu la kuhakikisha mwanafunzi anapata chakula kipindi anachokuwepo shuleni ili kumfanya azidi kuelewa kwani baadhi hushindwa kufanya vizuri kutokana na njaa.
“Utoaji wa chakula sehemu zingine wameanza na uji,hili ni suala muhumu,siku moja muwaite wazazi kwenye kikao muwashindishe na njaa kuanzia asubuhi mpaka jioni ili waone umuhimu wa watoto kupatiwa chakula shuleni.
“Mwingine unamwelewesha lakini anaona serikali ina wajibu wa kufanya kila kitu ikiwemo kutoa chakula hapana, Serikali haiwezi kufanya kila kitu,” amesema Mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi huyo amesema mpaka sasa wamewasaidia vijana zaidi ya 3500 ambao kibajeti ni zaidi ya shilingi bilioni 3 kupata elimu ya ufundi bure bila malipo toka 2019 mpaka sasa kupitia chuo cha Tarime VTC Chenye usajili namba REG/NACTVET/0587 Kinachomilikiwa na Taasisi ya Professor Mwera Foundation.
Amesema pia wanawasaidia watoto yatima ambao wanaishi katika mazingira magumu kuanzia elimu msingi sekondari pamoja na vyuo vya ufundi.
“Tunafursa ya kusaidia wale wanaotoka katika mazingira magumu ili waweze kufikia malengo.Maisha haya tunaishi kwa ajili ya binadamu wenzetu.Mipango tunayoweka hatuwezi kufanikiwa pasipo kupitia kwa binadamu wenzetu.
Tunapotamani kushikwa mkono nasi pia lazima tushike mkono watu wenye uhitaji.. tutendee watu yale tunayotamani kutendewa pia.
“Haya tuliyofanya inawezekana tukashindwa kuona faida yake kwa sasa, lakini kizazi kijacho kitakuja kufurahi kwa haya tunayoyafanya kwa sasa.
“Sisi tunasisitiza vijana kujiunga na vyuo vya ufundi na mwaka jana zaidi ya vijana 500,000 waliofanya mitihani waliopata divison one mpaka three ni zaidi ya 150,000, division Four mpaka ziro ni zaidi ya nusu ya waliofanya mtihani,” amesema Prof.Mwera.
Amesema vijana hao wako wapi wanafanya nini, hivyo ni lazima wahakikishe wanaenda katika vyuo vya ufundi ambayo vitawasaidia kupata ujuzi badala ya kupotelea mitaani na kuingiza Serikali hasara ya kurasimisha mafunzo yaliyopatikana nje ya mfumo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Serikali kupitia Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeipatia kibali Taasisi ya Professor Mwera Foundation kuhamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi Stadi Nchi nzima kazi ambayo tayari inaendelea.