NA: ANDREW CHALE DAR ES SALAAM.
WAFANYAKAZI wapya 16 raia wa Marekani wa kujitolea wa Peace Corps wameapishwa kuanza huduma yao nchini kwa kufanya kazi na kuishi na jamii za Kitanzania katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Zanzibar ambako watahudumu kwa miezi 24 wakizisaidia jamii kushughulikia vipaumbele muhimu vya maendeleo, ikiwa ni pamoja na elimu, afya ya jamii na kilimo endelevu.
Hafla hiyo fupi ya kiapo imefanyika katika makao makuu ya Peace Corps Tanzania, Jijini Dar es Salaam, ikiongozwa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Balozi Battle na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Dk.Edith Rwiza, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Tanzania, Stephanie Joseph de Goes.
Wafanyakazi hao wa kujitolea 16 walioapishwa ni kundi la kwanza la wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps kuhudumu nchini Tanzania toka kuanza kwa janga la UVIKO-19 hapo Machi 2020 ambalo lililosababisha kurudishwa nyumbani kwa zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 7,000 kutoka duniani kote ikiwemo 158 kutoka Tanzania.
Aidha, kwa wiki 12 zilizopita, wafanyakazi hao wapya wa kujitolea wamekuwa wakipata mafunzo ya kina y utamaduni wa Kitanzania, lugha ya Kiswahili na ujuzi mahsusi kulingana na sekta watakazozitumikia.
Awali akizungumza katika hotuba yake, Dk. Rwiza aliielezea Programu ya Peace Corps kama kielelezo cha uhusiano wa karibu kati ya Marekani na Tanzania na kama urithi wa urafiki kati ya Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Marekani John Kennedy, ambaye ndiye muasisi wa Peace Corps.
Ambapo alitoa wito kwa wadau wote katika maeneo ambapo wafanyakazi hawa wa kujitolea watahudumu kuwapa msaada wa hali na mali ili kuwasaidia kushamiri katika utendaji kazi wao.
Akihutubia kabla ya kusimamia kiapo kwa wafanyakazi wapya wa kujitolea, Balozi Battle aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa wao ndio watakuwa sura ya Marekani kwa watu wengi watakaokutana nao.
“Watu watawakumbuka ninyi, kwa sababu mlitembea miongoni mwao, mlifundisha na kujifunza pamoja nao… ninyi mnawakilisha kile kilicho bora kabisa kuhusu Marekani, na mna fursa ya kuishi na kujionea kile kilicho bora kabisa kuhusu Tanzania.” Amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Tanzania, Stephanie Joseph de Goes alitoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania, Chuo cha Ualimu Korogwe na familia zilizoishi na wafanyakazi wa kujitolea kwa kuisaidia Peace Corps kuwapokea na kutoa mafunzo ya Kiswahili na utamaduni wa Kitanzania kwa wafanyakazi wapya wa kujitolea kwa mafanikio makubwa.
Aidha, Amesisitiza dhamira ya dhati ya Peace Corps kufanya kazi na Tanzania kwa moyo wa ushirikiano, unyenyekevu na heshima.
mwisho.