Home LOCAL MGAO WA MAJI BANEBANE KUPATA SULUHU

MGAO WA MAJI BANEBANE KUPATA SULUHU

Na: Neema Mbalamwezi

Tatizo la mgao wa maji uliodumu kwa kipindi kirefu katika maeneo ya Malikoka, Banebane, Kwa Maua, Malinda St, Katoma St, Kanisa Katoliki Anuarite, Jumba la dhahabu, Kanisa la Sabato na Luhanga, kata ya Kisukulu Wilaya ya Ilala limepata ufumbuzi.

Ni baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kutekeleza mradi mkubwa wa Maji Banebane utakaokwenda kuwanufaisha wakazi zaidi ya 2,000 utakapokamilika ambao utekelezaji wake ulianza Aprili 2023 na unategemea kukamilika Juni 2023.

Mradi huo unatekelezwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa maji kwa kuongeza msukumo wa maji na kuondoa mgao wa maji kwenye maeneo tajwa ambayo yamekuwa yakipata maji kwa mgao kwa mda mrefu.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Mkoa wa Kihuduma DAWASA Tabata, Mhandisi Ole Philemon amesema mradi unahusisha kazi ya ulazaji wa bomba la inchi 8 la kusambaza maji kwenye maeneo tajwa ya wateja kwa umbali wa mita 1,300 na umegharimu kiasi cha Shilingi milioni 80 hadi kumalizika kwake.

Amesema mradi unatekelezwa kikamilifu na kazi inayoendelea ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa mtandao wa kusambaza maji kwa wananchi ili waanze kupata huduma ya maji.

“Mradi huu unasambaza maji kupitia matenki matatu ya Kimara yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 38.” amesema Mhandisi Philemon.

“Kupitia uzalishaji huu, tunaimani tatizo la mgao wa maji itafika mwisho,” amesema.

Amesema utekelezaji wa mradi umeenda sambamba na zoezi la kuainisha maeneo yanayopitiwa na kunufaika na mtandao huo.

Akielezea manufaa ya mradi huu, Mwenyekiti wa Mtaa wa Banebane, Ndugu John Nyahenga amesema mradi una manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo hili kwa kuwa wakazi wengi huwa hawapati maji muda wote kutokana na msukumo mdogo.

Amebainisha utekelezaji wa mradi huo unaleta matumaini kwa wananchi wa maeneo haya kupata maji ya uhakika, na kuishukuru DAWASA kwa kuliona hili na kuanzisha mradi maalumu wa kuongeza msukumo wa maji kwenye eneo hili.

“Nipende kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali imesikia kilio chao na imeanza kazi ya kuboresha upatikanaji wa maji, katika eneo hili la Banebane.” amesema Ndugu Nyahenga.

Kwa upande wake, Magdalena Charles, Mkazi wa Banebane amesema kwa sasa wana imani na kazi inayoendelea kutekelezwa kwenye eneo lao kwa kuwa huduma itaenda kuimarika kwa kiasi kikubwa.

“Tunaishukuru sana DAWASA kwa jitihada za kutekeleza mradi huu kwani tumekuwa tukipata maji kwa mgao hali iliyosababisha kukosa maji mara kwa mara,” amesema Ndugu Magdalena.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here