Home BUSINESS MAJALIWA AZITAKA HALMASHAURI KUSHIRIKISHA WACHIMBAJI UANDAAJI WA SHERIA NDOGO

MAJALIWA AZITAKA HALMASHAURI KUSHIRIKISHA WACHIMBAJI UANDAAJI WA SHERIA NDOGO

*Asema katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022/2023 mchango wa sekta ya madini ni asilimia 9.7

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza halmashauri zote za wilaya na miji, kwenye maeneo yenye madini ziandae sheria ndogo (by-laws) kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya madini ili ziendane na Sheria ya madini.

Ametoa agizo hilo leo Jumanne (Mei 09, 2023) wakati akifungua Kongamano la Wachimbaji Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) kwenye ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza

“Wakurugenzi wa Halmashauri wekeni mifumo bora ya kuweka tozo hizo na kuondoa kero kwa wachimbaji wadogo, punguzeni utitiri wa tozo kwa kubuni vyanzo vingine mapato”

Amesema kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuweka mazingira bora katika sekta ya uchimbaji mdogo na tayari imeshaanza kufanya marekebisho ya baadhi ya Kanuni na Sheria ya Madini na kuboresha mazingira ya biashara.

“Lengo la kufanya haya yote ni kuwezesha wananchi hasa wachimbaji wadogo nchini na wadau mbalimbali kushiriki ipasavyo katika uchumi wa madini”

Akizungumza kuhusu mchango wa Sekta ya madini kwenye pato la Taifa Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa umeongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017, hadi asilimia 7.2 mwaka 2021. “Pia katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022/2023 mchango wa sekta ya madini ni asilimia 9.7”

Amesema kuwa Serikali kupitia sekta ya madini imeweza kukusanya shilingi bilioni 409.66 sawa na asilimia 85.43 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 479.51 katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2022/2023.

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya madini kuharakisha mchakato wa kutafuta ufumbuzi wa suala Madini ya Lithium mapema iwezekanavyo ili kuweka wazi viwango vya uongezaji thamani kwa madini hayo kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kurasimisha maeneo yenye milipuko ya madini ambapo katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023 zimetolewa jumla ya leseni 6,381, zikiwemo leseni 3,865 za uchimbaji mdogo wa madini (PML), leseni 1,649 za biashara ndogo ya madini (Brokers).

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini ambapo hadi sasa jumla ya viwanda vitatu vya kusafisha wa dhahabu (Gold Refineries) vimeanzishwa .Viwanda vyote kwa pamoja vinauwezo wa kusafisha dhahabu kilogramu 515 kwa siku. Viwanda hivi vipo katika Mikoa ya Geita, Mwanza na Dodoma na vinafanya kazi”.

Previous articleFCS YAJA NA MRADI WA ‘URAIA WETU’ KUCHAGIZA MCHAKATO KATIBA MPYA
Next articlePATA HABARI KATIKA MAGAZETI YA LEO MEI 10, 2023
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here