Home LOCAL LIONS CLUB WAUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KWA KUPELEKA VIFAA TIBA ,...

LIONS CLUB WAUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KWA KUPELEKA VIFAA TIBA , JENERETA HOSPITALI KOROGWE

Na: Mwandishi Wetu

MKUU wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga Jokate Mwegelo amelishukuru Shirika la Lions Club International katika juhudi zake za kuungana na Serikali katika kuboresha huduma ya afya wilayani humo.

Jokate ameyasema hayo wakati akikabidhiwa viti sita vya magurudumu ‘(wheelchairs)’, jenereta ya 10KVA pamoja na mashine sita za kidijitali kwa ajili ya kupimia mapigo ya moyo kwa ajili ya kutumika katika Hospitali ya Wilaya Korogwe.

“Tunalishukuru shirika hili kwa niaba ya wananchi wa Korogwe mkoani Tanga kwa kuguswa katika kuokoa maisha ya mama na watoto na vitu ambavyo wamewachangia vitaweza kusaidia Serikali kuboresha huduma za afya ambazo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa.

“Kama mnavyofahamu Serikali yetu imejikita katika kuboresha miundombinu mbalimbali na kutoa huduma hususani katika sekta ya afya ambapo tumeweza kujenga na kuboresha hospitali ya Wilaya ,kuongeza zahanati na vituo vya afya, zahanati nyingine zimeboreshwa na kupandishwa hadhi.”

Amefafanua kuwa wilayani Korogwe hakuna kata ambayo haina Zahanati ,vituo vya afya na hicho ambacho kimefanywa na Lions Club kinakwenda kuongeza kasi zaidi kwa yale ambayo tayari Serikali wamefanya kwa ajili ya wananchi wake.

Ameongeza shirika la Lions Club kwa kuunga mkono kwa asilimia zote Serikali ya awamu ya sita na wanaahukuru kwa jinsi ambavyo wamejitoa kwa ajili ya jamii.

“Nitumie fursa hii kuwaalika kuja katika mbio zetu za akina mama na najua hii haijawahi kufanyika nchini kwetu Tanzania kwamba wajawazito wanatembea na wanafanya mazoezi kwa pamoja na wanaungwa mkono na akina baba na akina mama.

“Hivyo sisi kama Mamathon Korogwe tutalifanya Mei 28 mwaka huu kuazia saa 12 asubuhi na tumelenga akina mama wajawazito kutoka vijiji vyetu zaidi kwani tunataka kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi na kutoa elimu juu ya afya ya mama na mtoto kabla hajapata ujauzito.

“Na kipindi chote akiwa mjamzito,akiwa ananyoshe na namna ya kunyonyesha lakini afya ya mtoto baada ya kujifungua ni muhimu sana, amesema Jokate na kufafanua Korogwe kuna historia ambayo si nzuri sana na inajulikana ya kutupa watoto wao…hivyo tutatumia siku hiyo kuzungumza.

Kwaupande wake Mwakilishi wa Lions Club International ambaye pia ndio Katibu Mkuu wa Shirika hilo Bhavika Sajan amesema ni kawaida ya shirika hilo kurejesha Kwa jamii, na wamekuwa wakihudumu hapa nchini tangu mwaka 1960.

Amesema licha ya kua wanatoa huduma katika njia nyingi lakini juhudi zao zimezikita katika maeneo makuu matano ili kuigusa zaidi jamii na maeneo hayo matano ni miongoni mwa mambo muhimu na yanayosumbua ulimwengu kwa kiasi kikubwa.

Amesema dira na malengo yao ni kurudisha kwa jamii inayowazunguka,huduma zao zimejikita katika maeneo kama vile mazingira, kupambana na njaa, kisukari, macho pamoja na Saratani kwa Watoto.

“Tunasema kua kila kwenye uhitaji basi Lions tupo na kadri tunavyokua pamoja ndivyo tunavyotoa huduma nyingi zaidi.Mchango wetu kwa leo ni Jenereta ya 10KVA, viti sita vya Magurudumu na mashine sita za kidijitali za kupima Presha.

“Tunatarajia kuendelea kushirikiana kwa ajili ya kusaidia jamii lakini tunawashukuru Arun wa Specialised Engineering (T) Ltd, Ukumbi wa Tarangini, Lions Club of DSM Incredibles na Lions Club of DSM Tanzanites kwa msaada wao waliotoa kwa ajili ya hospitali ya Korogwe.”

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here