Mwenyekiti wa Kamati maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu kutatua changamoto za Kibiashara nchini, Dkt. John Jingu akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichoketi leo Mei 27,2023 Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo Bw.Hamis Livembe akizungumza alipokuwa akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
Na: David Langa, DAR ES SALAAM
Kamati maalum ya kutatua changamoto za kibiashara nchini iliyoundwa na Waziri Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Khasim Majaliwa Majaliwa mapema leo tarehe 27 Mei, 2023 imehitimisha kazi ya kukusanya maoni ya wafanyabishara kutoka sekta mbali mbali Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Mei 27,2023 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt..John Jingu amesema kuwa kamati hiyo imeshafanya kazi yake kwa asilimia sabini (70%), na sasa kamati inatawanyika katika makundi mbalimbali katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuwafikia wafanyabiashara waliopo katika maeneo hayo.
DR.Jingu amesema leo ikiwa ni siku ya tisa tangu kamati ianze kazi yake, na kwamba kuna baadhi ya changamoto za kiutendaji ambazo mpaka sasa zimeshatatuliwa kama mizigo ya baadhi ya Wafanyabiashara iliyokuwa ikishikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeachiliwa na kusitishwa kwa vikosi vya Operasheni za ukusanyaji kodi kwenye soko la Kariakoo.
“wafanyabiashara wameshachukua mizigo yao na wengine wanaendelea kushughulikia jambo hilo ambalo limeleta matumaini kwa wafanyabiashara, tunashukuru kwa ushirikiano mkubwa kwa wadau wetu na wote tunaowatembelea wanatuambia tusimwangushe Mama’’ aliongeza Dr. Jingu.
Kwa upande wake Mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo Bw.Hamis Livembe ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa kuwajumuisha kwenye kamati hiyo, jambo linaloonesha Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu.
‘’Mara nyingi tumekuwa nje ya vyombo vya maamuzi lakini kwa sasa tunashirikiana na Serikali kutatua changamoto za wafanyabishara nchini’’ amesisitiza Bw.Livembe.
Kamati hiyo inagawanyika katika kanda tano ambazo ni Kanda ya Juu kusini, (Mikumi, Iringa, Makambako ,Mbeya na Tunduma), Kanda ya ziwa (Kahama ,Mwanza na Sirari), Kanda ya Pwani (Zanzibar, Lindi na Mtwara) Kanda ya Magharibi (Kigoma na Kagera), na Kanda ya Kaskazini yenye Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe 14 ambapo wajumbe saba ni wawakilishi wa wafanyabiashara nchini na wajumbe wengine wanatoka kwenye Idara na Wizara mbali mbali zinazohusika na Biashara nchini.