Home Uncategorized CHALINZE CEMENT WAKIMBILIA MAHAKAMA KUU KUPIGANIA USAJILI WAO BRELA 

CHALINZE CEMENT WAKIMBILIA MAHAKAMA KUU KUPIGANIA USAJILI WAO BRELA 

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya saruji ya Chalinze Cement, imefungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ili kumtaka Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA), kuirudisha mara moja kampuni hiyo katika daftari la kampuni zilizosajiliwa na kutambulika kisheria nchini.

Kesi hiyo namba 113, ya Mwaka 2023 imefunguliwa leo Mei 15, 2023 na Chalinze Cement kupitia kwa Mkurungenzi Mkuu wake Mohamed Hussein Bahdera.

Aidha kesi hiyo inasimamiwa na Kampuni ya wanasheria nguli kutoka Kampuni ya Mawakili ya Law Associate Co. Ltd.

Katika kesi hiyo, Chalinze Cement imeiomba Mahakama Kuu, kubatilisha haraka amri ya kuifuta Kampuni hiyo pasipo kufuata sheria za makampuni kama sheria inavyotaka.

Itakumbukwa, baada ya vuguvugu la mida mrefu kuhusu madai ya BRELA kuifuta kampuni hiyo, hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara ilithibitisha kufutwa kwa Chalinze Cement, kwa madai nyaraka zake zimegundulika kuwa za uongo wakati wa usajili na Wanahisa wa kampuni hiyo hawatambuliki.

Taarifa hiyo ilitolewa, Machi mwaka huu na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji, Bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu hoja za wabunge akihitimisha mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Hata hivyo, katika mkutano wa wanahabari uliofanyika jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita, Wakili Melchisedeki Lutema, amesema sakata hilo lilianza mara tu baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kibiashara ya Septemba 23, 2022 juu ya kuungana au kutokuungana kwa kampuni za saruji ya Twiga na Tanga, yalieleza wazi kuwa yamezuia kuungana kwa makampuni hayo na hayakutoa muda maalumu wa kuisha kwa uamuzi huo.

Aliongeza kuwa, katika mazingira hayo Chalinze Cement walijitokeza kupinga muunganiko huo ili kulinda maslahi ya walaji na mazingira ya usawa wa soko.

Akizungumzia kufutwa kwa kampuni ya Chalinze Sementi, Wakili huyo alieleza wameshangazwa na utaratibu uliotumika kwa kuwa wateja wake hawakupewa taarifa na sababu za kufutwa kwake.

“Chalinze ni kampuni iliyosajiliwa mwaka 2021 na inatambulika na Serikali ndiyo maana hata kwenye rufaa yetu iliunganishwa kwa kuwa Sheria inasema kama yamefanyika maamuzi ambayo mtu anaona kisheria yanaweza kuingilia maslahi yake, anaweza kulalamika.

“Na Chalinze ni mmoja wa watu waliooona maslahi yake yanaweza kuingiliwa ndiyo akalalamika na anaweza kulalamika na haijalishi kama ameanza kuzalisha au au laa,” alisema Wakili Lutema.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here