Home LOCAL WAZIRI NDUMBARO ATOA WITO KWA WIZARA,TAASISI ZA UMMA KUITUMIA TUME YA KUREKEBISHA...

WAZIRI NDUMBARO ATOA WITO KWA WIZARA,TAASISI ZA UMMA KUITUMIA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro ametoa wito kwa Wizara, Taasisi za Umma kuitumia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ili kuondokana na changamoto ya kufanya marekebisho ya sheria mara kwa mara.

Waziri Ndumbaro ametoa wito huo Jijini Dodoma wakati akipokea ripoti maalum kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani January Msoffe alipowasilisha ripoti kuhusu mapitio ya sheria zinazosimamia uchaguzi wa vyama vya siasa nchini na sheria zinazosimamia utoaji haki katika mahakama ya mwanzo.

“Hii itaepusha changamoto ya sheria kufanyiwa marekebisho mara kwa mara kwakuwa tume ina wataalam waliobobea katika tafiti za kisheia hivyo waitumie,”amesema Dk. Ndumbaro na kuongeza kuwa bila kufanya hivyo taarifa zao hazitapokelewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Awali akiwasilisha ripoti hiyo, Jaji Mstaafu Msoffe amesema kuwa ripoti ya Uchunguzi iliyofanywa na hiyo imebaini mambo 10 ikiwemo baadhi ya vyama vya siasa kutoweka utaratibu wa wazi wa kuwapata wagombea wa ubunge na madiwani wanawake viti maalum.

Ameeleza kuwa utafiti umebaini mfumo wa upatikanaji wabunge na madiwani wanawake viti maalum baadhi ya vyama havijaweka utaratibu wa wazi wa kuwapata wagombea hao na hivyo kusababisha malalamiko na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa viongozi hao.

Ameongeza kuwa baadhi ya wadau walieleza changamoto hizo ni pamoja na upendeleo, maslahi binafsi, ukabila, rushwa na rushwa ya ngono, katiba za vyama kuwabana wanawake, mfumo dume, tamaa ya madaraka, kutokuwa na ukomo wa viti maalum na kukosekana kwa uratibu mzuri na usimamizi wa wazi wakati wa uchaguzi ndani ya vyama,

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, utafiti unaonyesha kwamba changamoto hizo zinasababisha kuwepo kwa manung’uniko kutoka kwa wanawake kuwa haki haikutendeka kwa walio wengi.

Kwa upande wa mapitio ya sheria ya uendeshaji mashauri katika mahakama za mwanzo, amesema utafiti umebaini kuwa kanuni zinazotumika hazijabadilika na haziruhusu kupokelewa kwa ushahidi wa kieletroniki, mpya wakati kesi ikiendelea.

“Utafiti unabainisha kwamba Kanuni za Mwenendo wa Mashauri katika Mahakama za Mwanzo ni rahisi na zinatumiwa na wananchi bila ulazima wa hudumaza uwakili. Kanuni hizo zimetumika kwa muda mrefu, zimezoeleka na zimethibitisha uwezo wa kutenda haki kwa wakati na kwa gharama nafuu.”amesema Jaji Mstaafu Msoffe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here