Home LOCAL WAZIRI MKUU: SERIKALI KUWEKA MFUMO MPYA MIKOPO YA ASILIMIA 10

WAZIRI MKUU: SERIKALI KUWEKA MFUMO MPYA MIKOPO YA ASILIMIA 10

*Ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia*

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezielekeza Halmashauri zote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo kwa makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu kuanzia Aprili hadi Juni, 2023 wakati Serikali inajipanga kuweka mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo.

Ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi Aprili 13, 2023) wakati akihitimisha hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wakijadili Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.

“Katika mkutano huu wa Bunge kuliibuka hoja kuhusu kiasi kidogo cha fedha za mikopo zitokanazo na asilimia 10 ya makusanyo ya Halmashauri kinachotolewa kwa makundi maalum kutokidhi matakwa ya kuyainua makundi hayo kwa kufanya shughuli za uzalishaji au biashara”

Katika hoja hiyo ilielezwa kuwa kumekuwa na changamoto kwenye baadhi ya Halmashauri kutoa fedha hizo kwa watumishi wa Halmashauri au wakati mwingine vikundi hewa badala ya walengwa na kusababisha fedha za mikopo hiyo kutorejeshwa.

Machi 29, 2023 wakati akipokea taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2021/2022 Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliagiza kuangaliwa upya kwa utaratibu wa utoaji wa mikopo ikiwemo kuangalia namna ya kutumia mabenki kupitishia mikopo hiyo.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri waheshimu na kuzingatia vipaumbele vinavyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo pamoja na kuhakikisha matumizi ya fedha hizo yanazingatia Sheria ya Mfuko wa Jimbo.

Vilevile, amemuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ahakikishe kuwa Maafisa Manunuzi kwenye Halmashauri hawawi kikwazo katika kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vya matumizi ya fedha za mfuko wa Jimbo hususan upatikanaji wa vifaa kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma Sura ya 410.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here