Home LOCAL WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO SITA KWA TAMISEMI, TOA

WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO SITA KWA TAMISEMI, TOA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa maagizo sita kwa viongozi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na Umoja wa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri unaohusika na maboresho ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) yatakayosaidia kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Ametoa maagizo hayo leo mchana (Jumanne, Aprili 4, 2023) wakati akifungua Mkutano wa 13 wa TOA (Tanzania Local Government Reforms Association) ulioanza leo kwenye ukumbi wa Jiji, Mtumba, jijini Dodoma.

Akizungumza na washiriki wa mkutano huo wa siku tatu kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amewataka viongozi na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe kunakuwa na ushirikishwaji wa karibu wa wananchi katika kuainisha changamoto zinazowakabili na kuwawezesha kupanga na kutekeleza afua za kukabiliana na changamoto hizo kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka.

“Kwa kufanya hivyo, tutaweza kutekeleza kwa tija, dhana ya ugatuzi wa madaraka sambamba na kuhakikisha maendeleo yanayopatikana kwa wananchi yanakuwa dhahiri na endelevu,” amesema.

Pia ameitaka Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ihakikishe Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka inakamilika mara moja ili iwezeshe taasisi zote nchini kupata mwongozo wa namna ya kutekeleza dhana hii muhimu kwa utoaji wa huduma na maendeleo ya wananchi.

“Vilevile, Ofisi ya Rais – TAMISEMI iendelee kufanya kazi kwa pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango kushughulikia suala la Ruzuku ya Serikali za Mitaa (LGDG) sambamba na utatuzi wa changamoto mbalimbali za utekelezaji wa miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa,” amesema.

Ili kuwajengea uwezo wanachama wake, Waziri Mkuu ameitaka TOA iendelee kuweka mikakati ya kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria ikiwa ni pamoja na mifumo ya utatuzi wa migogoro sambamba na ushirikishaji wananchi katika maamuzi na mipango ya maendeleo.

“TOA iwajibike kuhimiza wanachama kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatoa taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti ikiwemo taarifa za mapato na matumizi ili kujenga imani ya wananchi kwa Serikali yao.”

Pia ameitaka TOA iweke kipaumbele kwa wanachama wake katika kuandaa mikakati ya usimamizi wa miradi ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kazi zinazofanywa ziwe na ubora na zilingane na fedha inayotumika.

“Kwa nafasi zenu, wekeni mikakati ya ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya ndani ili kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii. Hii iwe sambamba na kubuni vyanzo vipya vya mapato, kufanya mapitio ya viwango vya ushuru na kuwa na takwimu sahihi za walipa kodi,” amesisitiza.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema anatambua wapo watumishi wengi walionufaika na mpango wa mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa Osaka, Japan kuanzia mwaka 2002. Amesema anaamini waliopata bahati ya kuhudhuria mafunzo hayo, wameona na kujifunza kuwa Wajapan wanayo mifumo thabiti ya kuwashirikisha wananchi na kujenga uwezo kwa mamlaka zao za Serikali za Mitaa ili ziwahudumie ipasavyo.

“Nitumie fursa hii kuishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kutuunga mkono. Itakumbukwa kuwa, wenzetu hawa walifanya hivyo licha ya kuwa nao walikuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali hasa umaskini kama ilivyo kwa Taifa letu.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Angellah Kairuki aliwataka Ma-RAS na Ma-DED watumie vema Mfumo wa Fursa na Vikwazo ulioboreshwa (yaani improved O&OD) ili kuongeza uwazi zaidi na uwajibikaji na hasa katika maeneo ya vitogoji, vijiji na mitaa.

Alisema kupitia mafunzo yaliyofadhiliwa na JICA, watumishi 6,367 walipata mafunzo ya namna bora ya ugatuaji wa madaraka kuanzia ngazi ya msingi na kwamba kupitia fursa hiyo, wataendelea kuboresha Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TOA, Bw. Albert Msovela ambaye pia ni RAS wa Kigoma alisema kupitia TOA wameweza kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ngazi ya msingi, utekelezaji wa LRGP I & II na matumizi ya Mfumo wa Fursa na Vikwazo ulioboreshwa (yaani improved O&OD).

Pia aliiomba Serikali irejeshe ruzuku ya LDGC ili iweze kuzisaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kama ilivyokuwa awali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here