Home LOCAL WAZAZI NA WALEZI KIJIJI CHA PWAGA, MPWAMPWA KUPATIWA ELIMU YA LISHE

WAZAZI NA WALEZI KIJIJI CHA PWAGA, MPWAMPWA KUPATIWA ELIMU YA LISHE

Na: Majid Abdulkarim, WAF – Mpwapwa

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma Mhe. Sofia Kizigo ametoa wito kwa Wazazi na Walezi kushirikiana na wataalamu wa lishe ili waweze kupatiwa elimu ya lishe pamoja na huduma mbalimbali zinazohusiana na afya.

Mhe. Kizigo ametoa wito huo leo kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI) Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu ambapo amesema lengo la kuwapatia elimu wazazi na walezi ni waweze kushiriki katika kusimamia lishe za watoto wao na kutengeneza kizazi chenye lishe bora kwa taifa la Tanzania.

Akizungumza Mhe. Kizigo amesema maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI) hufanyika kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika katika siku hiyo ambayo utekelezwa kila baada ya miezi mitatu.

“Katika Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI) kumekuwa kunatolewa huduma mbalimbali zinazohusu masuala ya afya na lishe na kina mama wengi wamekuwa wakiudhuria kupata huduma hizo huku kina baba wakiwa nyuma, hivyo ni jukumu lao kushirikiana na akina mama na kuhakikisha watoto wao wanapatiwa huduma hizo ili kuepika udumavu katika familia zao”, ameeleza Mhe.Kizigo.

Amesisitiza kuwa ili kutengeneza kizazi chenye lishe bora kinachotakiwa katika taifa ni lazima kuwekeze kwenye lishe na kuhakikisha wazazi na walezi wanapata elimu sahihi ya lishe ambayo itatusaidia katika kutengeneza kizazi chenye lishe bora.

Aidha amewataka wanawake wanapohisi wajawazito kuanza kuhudhuria kliniki mara moja, ili kuhakikisha siku 1000 za makuzi ya mtoto zinazingatiwa na kuwezesha kuwa na taifa lenye watu wenye afya na lishe bora na kuweza kufikia malengo endelevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema ameeleza lengo la ziara ya Mhe.Waziri kushiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI) ili kuweza kujionea shughuli zinazofanyika katika siku hiyo, na namna gani zimekuwa zikisaidia katika utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe.

Dkt. Germana ametoa rai kwa Mhe. Kizigo kuhamasisha jamii ya watanzania juu ya umuhimu wa lishe bora kwani lishe ndiyo msingi wa kila kitu, na hatuwezi kuwa na maendeleo kama wananchi wake hawana lishe bora.

Previous articleYASEMAVYO MAGAZETI YA LEO IJUMAA APRIL 7-2023
Next articleMAKAMU WA RAIS KATIKA KUMBUKIZI YA MIAKA 51 YA KIFO CHA SHEIKH KARUME
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here