Home BUSINESS TUNA MATARAJIO MAKUBWA NA STAMICO- KAMATI YA BUNGE

TUNA MATARAJIO MAKUBWA NA STAMICO- KAMATI YA BUNGE

 Mapato ya ndani yafikia shilingi Bil 38.7 kutoka bil 1.36

Lapata Leseni 6 Mpya, 4 za Madini ya Kimkakati

Asteria Muhozya na Tito Mselem- Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema inayo matarajio makubwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika kuibua wachimbaji watanzania na kuongeza ushiriki wao katika uchumi wa madini kutokana na mafanikio makubwa ambayo shirika hilo limeonesha ikilinganishwa na ilivyokua awali.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati Dunstan Kitandula Aprili 15, 2023 katika mahojiano maalum wakati kamati hiyo ilipopata fursa ya kujengewa uelewa kuhusu majukumu ya shirika hilo kwa lengo la kuiwezesha kamati hiyo kuisimamia na kuishauri Serikali ipasavyo.

Pamoja na kupongeza mafanikio yaliyofikiwa na STAMICO, amelitaka kuweka nguvu katika uwekezaji wa madini ya kimkakati na uendelezaji wa madini ya vito na kueleza kuwa ni maeneo muhimu ambayo STAMICO inatakiwa kuyafanyia kazi ili kuongeza mchango wa madini hayo katika maendeleo na uchumi wa taifa.

‘’Ukilinganisha na tulipotoka shirika hili sasa linafanya vizuri sana, tunaishukuru Serikali inatusikiliza na STAMICO wanatusikiliza kutokana na ushauri na maoni tunayowapatia, kiu yetu kubwa ni kutaka kuona shirika hili linazalisha wachimbaji wengi watanzania badala ya kutegemea wageni pekee.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza katika mahojiano hayo amesema shirika hilo limepata mafanikio mengi ikiwemo kuongeza mapato ya ndani kutoka shilingi bilioni 1.36 mwaka 2018/19 hadi kufikia shilingi bilioni 38.7 mwaka 2021/22.

Waziri Biteko amesisitiza kuwa, moja ya mikakati ya Wizara ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanawezeshwa kikamilifu kupitia STAMICO ili wakue na hatimaye kuongeza ushiriki wa watanzania katika shughuli za madini na kuwaondoa kwenye umaskini.

Ameongeza kuwa, wizara imejipanga kuhakikisha watanzania na taifa wananufaika ipasavyo kupitia madini ya kimkakati na kueleza kuwa maeneo mengi ya nchi yamebarikiwa kuwa na madini hayo na wizara inajipanga kufanya tafiti za kina kubaini kiasi kilichopo.

Pia, ametumia fursa hiyo kulipongeza shirika hilo na kueleza kwamba, ni taasisi ambayo inabuni mambo mapya kwa haraka na kuonesha tija tofauti na ilivyokua awali ambapo shirika hilo liliwekwa katika orodha ya mashirika yanayopaswa kufutwa na serikali.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali akifafanua kuhusu namna wizara ilivyoshughulikia changamoto za mlolongo mrefu wa taratibu za manunuzi ambazo kwa kiasi flani zinakwamisha utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo ambalo linajiendesha kibishara, amesema tayari serikali imekwisha kulitolea maamuzi na wizara inalifanyia kazi kwa karibu.

Awali, akiwasilisha mada katika semina hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amewaeleza wajumbe wa kamati kuwa shirika hilo limepata kandarasi kubwa tatu za uchorongaji zenye thamani kubwa kupitia Mgodi wa Dhahabu Geita wa shilingi bilioni 55.2, mgodi wa Buckreef shilingi bilioni 3.36 na Minerstation shilingi milioni 600 na kuongeza kwamba, hadi sasa shirika hilo linamiliki mitambo 16 ya kisasa ya uchongaji.

Akizungumzia nafasi ya shirika hilo katika uendelezaji wa madini ya kimkakati amesema limepata jumla ya leseni Sita mpya ambapo kati yake, leseni Nne ni za madini ya kimkakati yakihusisha madini ya lithium, kinywe (graphite) REE na copper.

Aidha, kutokana na namna shirika hilo linavyotekeleza majukumu yake, kutokana na muundo wake ambao unagusa mnyororo mzima wa shughuli za madini, muundo STAMICO unatajwa kuwa wa kipekee miongoni mwa mashirika ya umma Afrika ikilinganishwa na mashirika ya umma kama Angola, Zambia, Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo.

Akizungumzia mipango ya baadaye ya shirika hilo, Dkt. Mwasse ameitaja baadhi kuwa ni pamoja na kuanzisha mgodi mpya wa STAMICO ambao utamilikiwa na shirika hilo kwa asilimia 100. Pia, amesema mikakati mingine ni pamoja na kuzalisha kwa wingi mkaa mbadala wa Rafiki briquettes na kuongeza mitambo mikubwa ya uzalishaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here