Home BUSINESS THE ROYAL TOUR YALIPA, WATALII ZAIDI YA 300 WAWASILI

THE ROYAL TOUR YALIPA, WATALII ZAIDI YA 300 WAWASILI

Na: Beatrice Sanga-MAELEZO

Tanzania imepokea meli ya kitalii kutokea Miami nchini Marekani iliyobeba zaidi ya watalii 300 na wahudumu zaidi ya 300 ikiwa ni mwendelezo wa matokeo ya Filamu ya Royal Tour iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa malengo ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii

Akizungumza wakati wa kupokea wageni hao April 17, 2023 kwenye Bandari ya Dar es salaam Mkurugenzi Mkuu wa Bandari hiyo Mrisho Selemani amesema Mamlaka ya Bandari imefurahi kupokea meli ya aina hiyo, (Cruise ships) ambazo hufanya ziara zake za kitalii katika mataifa mbalimbali lakini pia ameongeza kuwa bandari imejipanga vizuri kuhudumia meli hizo za watalii huku ikiweka malengo makubwa ya kujenga eneo maalum la kuhudumia meli hizo.

“Sisi bandari kufuatia kuwepo kwa meli hizi za kitalii, tumejipanga kujenga eneo maalum kwa ajili ya kuhudumia meli hizi kwani itatupa fursa nzuri ya kukuza uchumi wetu pamoja na kuongeza uwepo wa meli kama hizi za kitalii kwani eneo tutakalojenga litakuwa na kila kitu ambacho kitamhudumia mtalii kabla ya kwenda kwenye vivutio vyetu.”

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mikutano na Watalii Bodi ya watalii Liliani Fungamtama amesema kuwa, watalii hao wamekuja kwa malengo ya kutalii kwenye vivutio hapa nchini ambao kati yao wengine wameenda Zanzibar, Serengeti na wengine wamebaki hapa kwa ajili ya kutembelea maeneo ya vivutio vilivyopo ikiwa ni pamoja na kupita Soko la vitu vya asili Mwenge Vinyago na kwenye fukwe zilizopo jijini Dar es Salaam.

Amesema uwepo wa watalii hao hapa nchini ni katika juhudi za kumuunga mkono Rais Samia katika filamu yake ya The Royal Tour na kusisitiza kuwa jambo hilo litasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini kwani malengo ni kufikia watalii milion 5 hadi ifikapo mwaka 2025.

“Yote hii ni kumuuunga mkono Rais wetu kwani sisi tunamhesabu kama Tour Operator namba moja katika kutangaza muendelezo wa filamu yetu ya The Royal Tour na itasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini na kufikia lengo tulilojiwekea,” ameongeza Fungamtama

Naye nahodha wa meli hiyo Kyraikos Karras amesema safari ilianza January 6, Mwaka huu kutokea Miami kupitia bahari ya Pacific hadi kufikia Dar es Salaam hii leo, huku wakitarajia kukamilisha safari yao May 27 huko nchini Hispania katika jiji la Barcelona.

Watalii hao wanatarajiwa kuongeza pato la taifa na kukuza uchumi wa nchi hivyo kurahisisha upatikanaji wa fedha za kigeni na kuchochea shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini.

Meli hiyo inatarajiwa kuondoka hapo kesho kuelekea nchini Afrika Kusini, ikumbukwe kuwa Novemba mwaka jana bandari ya Dar es Salaam pia ilipokea Meli ya kitalii ya Zaandam inayomilikiwa na Kampuni ya Holland America Line ikiwa na watalii 1060 ikiwa ni sehemu za safari za kitalii za meli hiyo kuelekea sehemu mbalimbali duniani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here