Na: WAF – Dar Es Salaam.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Afya imepiga hatua kubwa kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria na kufanikisha kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa leo kwenye maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani ambayo Kitaifa imefanyika Jijini Dar Es Salaam katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
“Tumepiga hatua kubwa kwenye mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria, tumeweza kupunguza kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 15.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022″ amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Mhe Majaliwa amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya malaria duniani kwa mwaka huu (Wakati wa kutokomeza Malaria ni sasa, Badilika, Wekeza, Tekeleza) inatakiwa itekelezwe kwa vitendo kwa kuwa inaenda sanjari na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na utekelezaji wa mkakati wa Serikali kwenye Mapambano dhidi ya Malaria.
“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imetoa maelekezo kwa Serikali, kuendelea kuihamasisha jamii juu ya matumizi ya vyandarua vilivyowekwa dawa, kupulizia viuwatilifu ukoko kwenye nyumba, kutekeleza mpango wa kuangamiza viluilui vya mbu na kutoa hamasa katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza” amefafanua Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesema kila mmoja ana mchango katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria hvyo ni vyema kila mmoja ajitathmini katika mapambano haya ili kufikia azimio la ‘Ziro Malaria inaanza na mimi’
Katika kutelekeza kwa Vitendo mapambano dhid ya ugonjwa wa malaria, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa unafuu kwa watanzania kwa kupata huduma za tiba ya ugonjwa wa malaria bure, ikiwemo Vipimo vya MRDT, Dawa za Aru, Sindano ya Malaria kali, Dawa za SP kwa ajili ya kutibu Malaria kwa wajawazito vyote vitatolewa bure kuanzia sasa.
Awali akizungumza, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imeendelea na mapambano dhidi ya kutokomeza ugonjwa huo na hadi kufikia mwaka 2022, idadi ya Mikoa yenye kiwango cha maambukizi ya malaria chini ya asilimia moja imefikia 9 (Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Iringa, Dar es Salaam, Songwe na Mwanza) kutoka Mikoa 6 mwaka 2017 hivyo kufanya asilimia ya watu wanaoishi katika maeneo yenye malaria chini ya asilimia moja kufikia asilimia 41.
Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka kipaumbele kikubwa kwenye mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria ifikapo Mwaka 2030 hivyo ni vyema Wadau wa Sekta ya Afya kwenye mapambano dhidi ya Malaria wakaunganisha nguvu za pamoja na Serikali katika utekelezaji wa afua za mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kuweza kuutokomeza nchini.
Mwisho.