Home BUSINESS STAMICO KUWAKUTANISHA WACHIMBAJI WADOGO NA WADAU WA MADINI YA VIWANDA

STAMICO KUWAKUTANISHA WACHIMBAJI WADOGO NA WADAU WA MADINI YA VIWANDA

Na; Beatrice Sanga MAELEZO

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) litawakutanisha Wachimbaji Wadogo na Wadau wa Madini ya Viwandani katika mkutano unaotarajiwa kufanyika kuanzia kesho Tar 5 na 6 April 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam na unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 700.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo April 4, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Dkt. Venance Mwasse, ameeleza kuwa mkutano huo utahusisha wadau mbailimbali wakiwamo wachimbaji wadogo wanaojihusisha na uchimbaji wa madini ya viwandani, wenye viwanda wanaotumia madini hayo pamoja na Taasisi za kifedha hapa nchini 

Dkt Mwasse ameongeza kuwa mkutano huo una lengo la kuwakutanisha kwa pamoja kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba wachimbaji wadogo wa madini ya viwandani na kujua sababu zinazowafanya wamiliki wa viwanda kutumia malighafi za nje lakini pia kuhakikisha malighafi zetu zinazalishwa na kutumika kwa tija ili kukuza maendeleo ya viwanda na nchi kwa ujumla

“Kwenye mkutano wa kesho na kesho kutwa ni kwa ajili ya hao wadau watatu niliosema kuwakutanisha na kujua changamoto zao zinazosababisha viwanda vyetu vinatumia marighafi kutoka nje wakati sisi tunazo na wote mnafahamu tunatekeleza ajenda ya viwanda na maendeleo ya viwanda, manufaa ya ajenda hiyo itakuwa na manufaa Zaidi kama tutatumia mali zetu wenyewe na uzuri ni kwamba mungu ametubariki tuna rasilimali hizo za madini kila mahali sasa tunataka kuhakikisha kwamba zinavunwa kwa wingi na kwa tija ili kuwa chanzo cha kuendeleza maendeleo ya nchi ”Dkt. Mwase

“Nichukue nafasi hii nitoe wito kwa watanzania wote wachimbaji wadogo, wenye Taasisi za Fedha, wenye viwanda vinavyotumia madini ya viwandani waje kwa wingi kwenye huu mkutano wetu. Kwa namna ambavyo tumejipanga kila atakayekuja tutahakikisha kwamba atatoka na kitu ambacho kitaenda kusaidia kupeleka mbele shughuli anazozifanya na biashara anayoifanya” Amesema Dkt. Mwase

Naye, Mkurugenzi mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Leodegar Tenga amesisitiza matumizi ya malighafi yanayozalishwa nchini ili kukuza uchumi wetu na kupunguza gharama zinazotumika kuagiza malighafi kutoka nje ya nchi

“Nchi yetu kama tunavyofahamu ni nchi inayotaka kujenga uchumi wa viwanda na mkutano wa kesho ni katika muendelezo wa hiyo dhana ya kujenga uchumi wa viwanda tuna madini yetu nchini sasa tunawajibu sisi kama sisi CTI kuhamasisha wanachama wetu ambao ndo wenye viwanda na wale ambao wanasaidia maendeleo ya viwanda tufanye kila linalowezekana kutumia malighafi za ndani ya nchi” Amesema Bw. Tenga.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here