RAIS Samia Suluhu Hassan amemwagiwa sifa na wananchi na viongozi mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kuchukua hatua za haraka na madhubuti kushughulikia uzembe na ubadhirifu wa pesa za umma uliobainishwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu Jumapili, Rais Samia alivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli la Tanzania (TRC) na kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Mhandishi John Nzulule.
Aidha, Rais Samia amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi kuwaelekeza Makatibu Wakuu wote wa wizara pamoja na Watendaji Wakuu wa taasisi za serikali kusoma ripoti zote za CAG za mwaka wa fedha 2021/22 zilizotolewa hadharani Aprili 6 mwaka huu, kujibu na kuzifanyia kazi hoja zote zilizoibuliwa.
“Watendaji wote watakaobainika kuhusika na uzembe au ubadhirifu wachukuliwe hatua za kisheria,” imeeleza sehemu ya taarifa ya Ikulu.
Hatua hizo za Rais Samia zimeibua shangwe za wananchi nchini Tanzania na hata kuwagusa wananchi wa nchi za jirani za Kenya na Uganda ambao wametoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii.
“Natamani huyu Mama (Rais Samia) angekuwa Rais wetu, Kenya tungekuwa sawa sana,” alisema raia wa Kenya, Jibril Ndiema, kupitia Twitter.
Wananchi kadhaa wa Uganda na Kenya walitoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii wameweka bayana shauku yao ya kuwa na Rais kama Samia ambaye anachukua hatua za hadharaka na madhubuti dhidi ya tuhuma za ufisadi serikalini.
“Ikulu ya Kenya tunawaomba tafadhali mchukue hatua kama hizi za (Rais Samia) kwa Shirika la Ndege la Kenya,” alisema Donald Omoro, raia wa Kenya, kupitia akaunti yake ya Twitter ya @DonaldKOmoro1.
Naye Farhiya Abass, mfanyabiashara anayeishi Mombassa, Kenya, alisema kupitia akaunti yake ya Twitter @farhiyaabass kuwa:“Mama Suluhu hana mchezo kabisa.”
John Luke Tambiti, Mkurugenzi Mtendaji, wa taasisi isiyo ya kiserikali ya INUA Initiative Uganda, naye alitoa sifa kwa Rais Samia kuonesha uongozi mahiri kwa kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa umma waliohusika na uzembe na ubadhirifu kwenye ripoti ya CAG.
“Kwa Uganda, kwetu hii ni ndoto tu (kupata Rais anayechukua hatua dhidi ya ufisadi). Huku kwetu wezi ndiyo kwanza wanazawadiwa nafasi kubwa zaidi,” alisema kupitia akaunti yake ya Twitter ya @LukeTambiti.
Hapa nyumbani, wananchi wa sehemu mbalimbali nchini nao wameonesha hisia zao za kuvutiwa na hatua za Rais Samia kuagiza ripoti ya CAG ifanyiwe kazi kikamilifu na makatibu wakuu na watendaji wengine wa serikali.
“Kwa kweli Rais Samia amejibu kilio chetu wananchi cha kutaka kuona hatua kali zinachukuliwa dhidi ya watumishi wa umma wachache wanaofuja pesa za umma. Tungependa tuone wabadhirifu wote wanafukuzwa kazi na wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma dhidi yao,” alisema Francis Mwenegoha, mwanafunzi wa chuo anayeishi Morogoro.
Naye Shomari Msabaha, fundi ujenzi wa Dar es Salaam, amemtaka Rais Samia kutorudi nyuma katika mapambano dhidi ya ufisadi.
“Sisi wananchi wa Dar es Salaam tunaunga mkono juhudi za Rais Samia kupambana na ufisadi na tunamtaka asonge mbele, tuko naye bega kwa bega kwenye vita hii,” alisema.
Asha Bakari, Mama Lishe wa mkoa wa Mwanza, alimuomba Rais Samia awadhibiti maafisa wa Manispaa na Halmashauri za miji na wilaya ambao wanafanya ubadhirifu kwenye pesa za kuwakopesha vikundi vya kina mama.
“Serikali kila mwaka inatoa pesa kwa ajili ya kutukopesha sisi kina mama wa hali ya chini kupitia vikundi vyetu, lakini pesa hizi zimekuwa zinaliwa na maafisa wa umma wasio waaminifu na hazifiki kwetu. Tunamuomba Rais Samia akomeshe huu ubadhilifu,” aliongeza.