Home Uncategorized KITUO CHA AFRIKA MASHARIKI CHA MAFUNZO YA ULINZI NA USALAMA WA VIMELEA...

KITUO CHA AFRIKA MASHARIKI CHA MAFUNZO YA ULINZI NA USALAMA WA VIMELEA CHAFUNGULIWA NCHINI

 Na: Catherine Sungura,Dar es salaam

Serikali itaendelea kuboresha huduma za Maabara zote nchini kwa kuzingatia matakwa ya ulinzi na usalama wa Kibiolojia na kuhakikisha usalama wa watenda kazi pamoja na mazingira yote kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo Aprili 3, 2023 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kuwa kituo cha Kikanda cha Afrika Mashariki cha Mafunzo ya ulinzi na usalama wa vimelea jijini Dar es Salaam.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha usalama wa afya za Watanzania na wote waishio ndani ya mipaka ya Tanzania inalindwa. “Wizara inatekeleza viwango vya Kitaifa na Kimataifa kuhakikisha vimelea hatarishi vinavyotokana na hatua za upimaji na tafiti ndani ya maabara havisambai katika jamii na kuleta madhara kama vile milipuko ya magonjwa”.

Amesema kuteuliwa kwa kituo hicho kunadhihirisha jinsi maabara ya Taifa ya Jamii inaendelea kauminika duniani na kuwa na uwezo wa kupima vimelea vyote hatarishi kwa kuwa vimelea hatarishi vinaweza kutoka kwa wanyama kwenda kwenye mazingira na baadaye kuathiri afya ya binadamu.

“Utekelezaji wa afua ya ulinzi na usalama (Biosafety and Biosecurity) ni suala mtambuka baina ya Wizara mbalimbali nchini hivyo tunahitaji kuwajengea uwezo wataalamu wetu, kupitia kituo hiki tutapata fursa ya wataalamu wetu wa Tanzania kupata mafunzo ya kimataifa kwa gharama nafuu kwani mafunzo hayo yatakuwa yanafanyika hapa hapa nchini”. Aliongeza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema tangu kutangazwa kwa kituo hicho wamekwishapokea maombi toka Chuo Kikuu cha Musinde Murilo nchini Kenya ya kuleta wanafunzi wanaochukua shahada ya ulinzi na usalama wa vimelea kwa ajili ya elimu kwa vitendo na kudhihirisha kwamba maabara inaaminika na inayo uwezo.

Hata hivyo Waziri huyo amewashukuru wadau wa Afrika CDC pamoja na wadau wa maendeleo kwa ushirikiano wenye tija na thamani kubwa kwa Watanzania na kuwataka waendelee kutimiza wajibu wao ili sekta ya afya iendelee kuimarika kwa huduma bora kwa wananchi.

Naye, mwakilishi kutoka Afrika CDC Dkt. Talkmore Maruta ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwazi wa kutoa taarifa hususani ya ugonjwa wa Marburg na hivyo kuonesha namna nchi inakuwa salama na na kuongeza kuwa CDC itaendelea kushirikiana na Serikali na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya nchini katika kujiandaa, kutambua na kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Tanzania inaungana na nchi ya Afrika ya Kusini ambayo imekwishateuliwa kuwa kituo cha mafunzo kwa nchi za kusini mwa Afrika ambapo Tanzania iliwasilisha maombi ya kuteuliwa kuwa kituo cha maombi mnamo Septemba 2022 na Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ilipata asilimia 100.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here