Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na Washereheshaji kupitia Chama Chao Cha Kisima cha Mafanikio (KCM) leo Aprili 4, 2023 jijini Dodoma wakati afungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama hicho.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa rai Kwa wadau wa Sekta za wizara yake kuzungumzia na kukemea mmomonyoko wa maadili katika jamii kwa kutumia taaluma na vipaji walivyonavyo.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa rai hiyo leo Aprili 4, 2023 jijini Dodoma alipofungua Mkutano Mkuu wa Chama Cha Washereheshaji cha Kisima cha Mafanikio (KCM) ambapo amesema wadau hao wana nafasi kubwa katika kuzungumza na kuisaidia jamii kuepuka masuala yanayokiuka maadili mema yakiwemo ya unyanyasaji, ukatili na mila ambazo sio za Kitanzania.
“Natoa Rai kwenu Waneni (MC’s) muendelee kuunga mkono juhudi za Serikali na mafanikio yake kwa kuendelea kutumia fursa zilizopo ikiwemo kupata mikopo nafuu kutoka Mfuko wa Utamaduni na Sanaa lakini pia kuwa mabalozi Wazuri wa Matumizi sahihi na sanifu ya Lugha ya Kiswahili” amesema Balozi Dkt. Pindi Chana.
Awali muanzilishi wa Chama hicho Bw. Brison Makene amesema mkutano huo una lengo la kukumbushana namna ya kuboresha kazi zao, kuzirasimisha pamoja na kubadilishana uzoefu.
Mkutano huo umewakutanisha Washereheshaji, Wahamishaji, Watunzi wa Fasihi na Wapambaji kutoka Kanda za Tanzania ikiwemo Kanda ya Kati, Magharibi, Mashariki na Kaskazini.