Home LOCAL ASKOFU MKUU KAT AKUMBUSHA WAKRISTO KUWA WAAMINIFU KUTEKELEZA MIRADI YA SERIKALI NA...

ASKOFU MKUU KAT AKUMBUSHA WAKRISTO KUWA WAAMINIFU KUTEKELEZA MIRADI YA SERIKALI NA AHADI ZA KANISA

  Na Maiko Luoga Tanga

Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Maimbo Mndolwa, amewataka Wakristo wanaopewa kazi na Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo nchini kutekeleza miradi hiyo kwa uaminifu na kiwango kinachostahili.

Alisema hayo wakati wa Adhimisho la Misa takatifu ya Sikukuu ya Mitende iliyofanyika jumapili Aprili 02, 2023 katika Makanisa ya Anglikana Mtakatifu Mathayo Hale na Kung’aa kwa Bwana Msambiazi Dayosisi ya Tanga.

Aidha alisema haipendezi kuona mradi wa Serikali upo chini ya kiwango aliyepewa fedha kutekeleza ni mkristo baada ya muda mfupi wa matumizi watanzania wanaendelea kupata adha ya ubovu wa miradi hiyo ikiwemo Barabara na miundombinu mingine.

“Ukristo sio koti unaloweza kulivua na kuvaa, ukristo ni maisha, haipendezi sana kumsikia muumini ambae anaheshima ndani ya Kanisa akapewa tenda na Serikali ya kujenga Barabara akajenga chini ya kiwango na akalipwa fedha zote”

“Haileti maana kusikia Mkristo mshiriki mzuri wa meza ya Bwana ama mzee wa Kanisa, anafika mahali anakwepa kulipa kodi, haiingii akilini kusikia Mkristo na muumini mzuri anaingia Kanisani kwa unyenyekevu mkubwa lakini akitoka hapo mlangoni utasikia ni Msagaji, Shoga au basha, humu Kanisani haonekani lakini akishatoka nje amevaa koti jingine”

“Tuwakumbushe mamlaka ya Kaisari haina maana kwamba ufanye vibaya na hii mamlaka ya Mungu haimaanishi kwamba ufanye vizuri huku pekee, mamlaka hizi mbili zinatembea pamoja ili kutufanya tuweze kuishi salama katika nchi”

“Tutumie nafasi hii kulikumbusha Kanisa, anae kwepa kulipa kodi ya serikali nisawa na asiyetoa sadaka Kanisani, mwizi ni sawa na mdokozi yeyote, katika safari hii Kristo anatukumbusha unyenyekevu wake, tunapoishi katika ulimwengu huu tunapaswa kujitoa nafsi zetu kwaajili ya utukufu wake” alisema Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here