Mwili wa binti ambaye mpaka sasa jina lake halijafahamika anaekadiliwa kuwa na umri kati ya miaka 18-20 umekutwa kando kando ya barabara ukiwa umetekelekezwa katika mtaa wa Mwembeni kata ya Nyankumbu halmashauri ya Geita mji Mkoani Geita.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kaimu Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Geita Kamishina Msaidizi wa Polisi Berthaneema Mlay amesema mpaka sasa chanzo cha kifo cha binti huyo hakijafahamika.
Kamanda Berthaneema amesema taarifa za tukio hilo zilitolewa na raia wema ambapo jeshi la polisi liliwasili katika eneo la tukio na kuchukua mwili huo kwa uchunguzi ambapo mpaka sasa mwili huo umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita.
“Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Geita kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi Kwa hiyo kama jeshi la polisi tunaendelea kutafuta chanzo cha kifo cha huyo mtu Lakini pia ndugu wakijitokeza tutafanya uchunguzi ili tuweze kujua kitu gani kimesababishia kifo chake mwili ulikutwa pembezoni mwa barabara hauna jeraha na mpaka sasa hivi ndugu hawajapatikana”.
Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Mwembeni akiwemo Elina Petro amesema eneo ulipokutwa mwili huo ni kando kando ya msitu wa miti inayomilikiwa na watu binafsi ambapo eneo hilo limekuwa tishio na kificho cha waharifu.
Wameiomba serikali kuchukua hatua kuwafichua waharifu wanaotumia msitu huo kama kificho huku akiwaomba wamiliki wa eneo hilo wavune msitu ili eneo libadilishiwe matumizi na kuwa la makazi.
“Matukio ni mengi yanayotokea hapa kwanza mimi mwenyewe hapa nilishawahi kuvamiwa sikuweza kupata msaada kwa sababu nimetazamana na hili pori, ilikuwa mwaka 2017.”