Home LOCAL SUA KUMUENZI HAYATI EDWARD MORINGE SOKOINE KWA VITENDO

SUA KUMUENZI HAYATI EDWARD MORINGE SOKOINE KWA VITENDO

NA: FARIDA MANGUBE MOROGORO.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetakiwa kujitathimini jinsi gani kinatekeleza majukumu yake yakiwemo kutoa mafunzo kwa vitendo, kufanya tafiti zitakazo saidia kupambana na changamoto za sekta ya kilimo pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi hayati Edward Moringe Sokoine.

Kila ifikapo Aprili 12 kila mwaka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kinaadhimisha kumbukizi ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo alisimamia kupitishwa kwa mswada wa sheria wa kuanzisha kwa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA, Prof. Amandus Muhairwa amesema lengo la kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine ni kuyatekeleza na kuyaenzi maono yake ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Amesema kwa mwaka huu 2023 SUA itaadhimisha kumbukizi ya Sokoine kuanzia Mei 23 hadi 26 kwa kufanya shughuli mbalimbali kama kufanya mkutano wa Kisayansi kwa ajili ya wanataaluma, watafiti, wanafunzi na wadau.

Kutoa huduma za tiba ya mifugo kupitia hospitali ya Taifa ya Rufaa ya wanyama ambapo ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro na mikoa jirani kupeleka mifugo yao ili kupata huduma ya matibabu na ushauri kutoka kwa wataalamu wa mifugo kutoka SUA.

Pia kutakuwa na maonyesho ya teknolojia na ubunifu katika kilimo, ufugaji na uvuvi, pamoja na mdahalo wa kitaifa utakaofanyika siku ya tarehe 26.

Prof. Samwel Kabote akizungumza kwa niaba ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma,Utafiti na Ushauri wa Kitaalumu amesema Hayati Edward Moringe Sokoine alikuwa kiongozi mwenye msimamo, mzalendo na fikra zenye mwelekeo wa juu wenye kuleta maendeleo kwa jamii.

“Hayati Sokoine alikuwa mtu anayesimamia vitu bila ya uoga, ikiwa ni pamoja na kujitegemea kwenye chakula, soko la kitaifa na maendeleo vijijini.” Alisema Prof. Samwel Kabote.

Amesema katika kumuenzi Moringe Sokoine, Chuo kikuu cha SUA kinafanya kazi ya kujitangaza ndani na nje ya nchi, kutoa fursa kwa wanataaluma na watafiti kujadili matokea ya tafiti mbalimbali ili kuisaidia serikali kuongeza uzalishaji wa mazao.

Kwa upade wao baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro akiwemo Bi. Mwajuma Ramadhani na Josephat Masawe wamewataka viongozi wa umma kuwa wazalendo na kuiga mfano wa Hayati Edward Moringe Sokoine kwani amekuwa kiongozi wa mfano na aliyeacha alama kwa taifa.

Previous articleCHIKOTA:NANYAMBA KUNA UPUNGUFU WA WATUMISHI WA AFYA 610
Next articleVideo Mpya : JANDO Ft DADY P & DASHIEE – KUKUPENDA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here