NA: TIMA SULTANI
TIMU ya Yanga imefanikiwa kutinga Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika kwakuwachapa wapinzani wao US Monastir mabao 2-0.
Mchezo huo wa marudiano umechezwa leo saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya mchezo huo yalifungwa dakika ya 33 na Kennedy Musonda huku la pili likiingizwa kimiani na Fiston Mayele kipindi cha Pili dakika ya 59 ya mchezo huo.
Mbali na kufuzu robo fainali mabao hayo yatawafanya Wanajangwani hao kujikusanyia milioni 10 zilizo ahidiwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassa ambaye ananunua mabao yote yanayofungwa katika kila mchezo wa kimataifa kwa timu za Tanzania.
Yanga wamefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali na kujiweka katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa kundi lao (D) kwa idadi ya magoli ya kufunga wakiwashusha wapinzani wao Monastir ambao wote wana point 10.