*Ataka wananchi watunze vyanzo vya maji, wawafichue waharibifu*
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema suala uhifadhi wa mazingira ni muhimu kwa nchi na akataka kila Mtanzania azingatie uhifadhi wa mazingira.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Machi 16, 2023) wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa sekta ya maji na mamia ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Mradi wa Ujenzi wa Mfumo wa Usambazaji Maji kati ya Makongo na Mji wa Bagamoyo uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Tegeta A, jijini Dar es Salaam. Pia alizindua Wiki ya Maji kwa mwaka 2023.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali za kuboresha miundombinu ya ukusanyaji na usambazaji wa maji, ni jukumu la kila Mtanzania kutunza vyanzo vya maji. “Tuna jukumu kubwa nalo ni la kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji; na eneo hili tuna mgogoro mkubwa kwani vyanzo vyetu vya maji vinaharibiwa, ni wajibu wetu kutunza vyanzo hivi.”
Amesema Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameshatoa mwongozo wa uhifadhi wa vyanzo vya maji na kila Mtanzania anapaswa kuzingatia hilo. “Tunahitaji kuweka nguvu moja katika kusimamia, kulinda, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za maji. Nitoe wito kwa Wizara, wadau wa maji na wananchi tutunze vyanzo hivi iwe ni visima, mito, au mifereji vyote tuvilinde.”
“Suala la uhifadhi ni muhimu sana. DAWASA isimamie suala hili kwa karibu na kutoa taarifa mapema. Wakurugenzi wa Mabonde ya Maji nchini kama vile Ruvuma, Rufiji, Malagarasi na mabonde mengine yote hakikisheni mnafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili vyanzo hivi visiharibiwe. Wananchi tulinde vyanzo hivi na mtu akionekana anaharibu, kama ni kisima au chanzo kingine, tuchukue hatua, tusisite kwa sababu huo ni uhujumu.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira iliyokuwepo, Waziri wa Maji. Jumaa Aweso alimwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Bw. Kiula Kingu ahakikishe wananchi wote walioomba maji wafungiwe mita ndani ya siku saba kama Mkataba wa Huduma ya Wateja unavyosema.
Akielezea utekelezaji wa miradi ya maji kwenye wizara yake, Waziri Aweso alisema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwenye wizara hiyo ambazo ni mahsusi kwa utekelezaji wa miradi ya maji. “Mheshimiwa Rais kwa sasa ametoa asilimia 90 ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maji, wakati awali utekelezaji ulikuwa ni kati ya asilimia 50 hadi 60 tu,” alisema.