WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua jengo la wagonjwa wa dharura kwenye hospitali ya wilaya ya Maswa ambalo limegharimu sh. milioni 311.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa Maswa waliofika kushuhudia uzinduzi huo leo mchana (Jumapili, Machi 26, 2023), Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ujenzi na kwamba jengo hilo ni zuri.
“Nimepita kwenye jengo lenu, ni zuri na nimekuta limejaa vifaa. Jengo hili limekuja kwa wakati muafaka kwa sababu kuna barabara kuu ambayo inapita hapa kwenye mji wenu,” amesema.
Waziri Mkuu alipouliza ni dharura gani zaidi wanazozipata, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. James Bwire alisema akinamama wanaojifungua zamani walikuwa wanaikosa huduma hiyo lakini kwa sasa inapatikana hapo. Pia alisema madereva wa bodaboda wanaongoza kwa ajali ambapo kwa wiki wanapokelewa majeruhi wanne.
Naye, Naibu Waziri (OR-TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange amesema jengo hilo lililozinduliwa ni miongoni mwa majengo 80 yaliyojengwa nchini kwa kutumia fedha za UVIKO-19 na kwamba katika mkoa wa Simiyu, yamejengwa pia katika wilaya za Bariadi na Itilima.
Naye, Mbunge wa Maswa Mashariki, Bw. Stanslaus Nyongo alisema katika mwaka huu wa fedha, wilaya hiyo imepokea zaidi ya sh. bilioni 30 ambazo zimejenga miundombinu mbalimbali likiwemo jengo hilo na kununua vifaa vya sh. milioni 400 ambavyo sasa hivi vimeanza kufanya kazi.
“Pia tumejenga vituo vya afya sita na tumemalizia maboma ya zahanati, tumejenga vyumba vya upasuaji vikubwa viwili vya kisasa kwenye hospitali hii, vyumba vya wagonjwa mahututi kwa watoto wachanga na watoto njiti na kununua x-ray mobile moja.”
Pia alisema wamenunua mashine moja kubwa ya x-ray ambayo pia ni ya kisasa lakini wameshindwa kuisimika kwa sababu jengo lililopangwa kutumika ni la zamani na wataalamu wa mionzi walisema kuta zake zinapitisha mionzi. Aliomba wapatiwe fedha za kujenga jengo jipya ili huduma hiyo ianze kutolewa kwa haraka.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa kiwanda cha chaki na vifungashio ambalo limegharimu sh. bilioni 8 na ujenzi wake umefikia asilimia 97.
Akijibu hoja zilizoibuliwa na Wabunge wa mkoa huo, Waziri Mkuu atafuatilia maombi yao ya sh. bilioni 2.8 za kukamilisha kiwanda hicho ili kianze kazi mara moja.
Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa, Bw. Simon Berege alimweleza Waziri Mkuu kwamba walipokea sh. bilioni 8.09 na fedha hiyo imetumika kujenga jengo la kiwanda cha chaki, jengo la kiwanda cha vifungashio, jengo la kiwanda cha kuchakata gypsum, ofisi ya kiwanda, ujenzi wa uzio na ununuzi wa mitambo ya kiwanda cha chaki.
Alisema ujenzi wa jengo la kiwanda cha vifungashio vya karatasi na plastiki umefikia asilimia 98 lakini wanahitaji sh. bilioni 20 ili waweze kukamilisha ununuzi wa mitambo. Alisema miradi hiyo itakapokamilika, inatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 250.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya Mkoa wa Simiyu kwa kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya ya Maswa.