Home BUSINESS WASAFIRISHAJI MKAA KWA BODABODA WANAVYOGEUZA VIJIJI KUWA ‘JANGWA’

WASAFIRISHAJI MKAA KWA BODABODA WANAVYOGEUZA VIJIJI KUWA ‘JANGWA’

 Na:  Said Mwishehe, Michuzi TV

WAKALA wa Huduma za Misitu(TFS)kwa kushirikiana na mamalaka nyingine za Serikali wamamua kujitosa kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaoendelea kufanywa kila kukicha.

Kwa sehemu kubwa uharibifu wa misitu unatokana na uvunaji mkaa usiozingatia taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.Ukweli hali ni mbaya misitu inaharibiwa, miti inateketea.

Ukitaka kuamini uharibifu mkubwa ambao umefanyika kwenye misitu yetu wala huna sababu ya kwenda mbali, kwa walioko mikoa ya Pwani na Dar es Salaam wanafahamu hili.

Ukiwa barabara ya Morogoro utaona misururu ya bodaboda ilivyobeba shehena za magunia ya mkaa.Ukienda Kisarawe nako hali ni mbaya zaidi, bodaboda zinapishana na magunia ya mkaa.

Wanaojihusisha na biashara hiyo hawana woga, hawana wasiwasi, wanaharibu misitu kwa kukata miti ili kutengeneza mkaa.Hali ni mbaya, tena ni mbaya mnooo.Ninaposema hali ni mbaya uwe unaelewa basi!

Kwa hatua iliyofikia , sote tunalojukumu la kupaza sauti na kusema sasa inatosha, tuungane kulinda misitu yetu, tuungane kulinda miti yetu,tuungane kulinda hifadhi zetu. Faida za uwepo wa misitu zinasemwa kila kukicha.Sina sababu ya kurudia.

Wakati natafari kuhusu uharibifu mkubwa wa misitu yetu unatokana na uvunaji mkaa haramu, macho na masikio yanafarajika kwa kuona hatua zinazochukuliwa na TFS kwa kushirikiana na Mamalaka za Serikali.

Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kuanzishwa kwa operesheni maalumu kukomesha uharibifu wa misitu na maeneo mengine ya hifadhi kwa kukata miti ili kuchoma mkaa.

Ndio operesheni hiyo imeanza kuzaa matunda, wafanyabiashara wa mkaa wanaotumia bodaboda wameanza kupungua barabarani, ile misururu yao mirefu hatuioni tena.Ni hatua ya kupingezwa , ni hatua ya kuunga mkono.

Hivi karibuni baada ya kuona wafanyabiashara ya mkaa kwa bodaboda wamepungua nikaamua kufunga safari kwenda baadhi ya vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini.

Vijiji vya Kimalamisale na Madege ni miongoni mwa vijiji ambavyo umefanyika uharibifu mkubwa, wananchi na viongozi wa vijiji hivyo wanakiri hali ni mbaya, miti imeteketea, vijiji vinabaki kuwa jangwa, kisa wafanyabiashara ya mkaa hususani wanaotumia bodaboda.

Hata hivyo wananchi wanafurahia jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mkoa wa Pwani na TFS Kanda ya Mashariki kupitia operesheni inayoendelea inayokwenda sambamba na utoaji elimu kwa wananchi kufahamu umuhimu wa kutunza misitu.

Ofisa Mtendaji Kijiji cha Kimalamisale Abdul Tengeneza na Mwenyekiti Salum Mtego wanaeleza kuwa kwenye kijiji hicho kumekuwa na uvamizi mkubwa wa watu ambao wameingia kijijini kukata miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa, hivyo wanaona TFS na Serikali kuchukua hatua ili kunusuru uharibifu wa misitu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Madege Idd Salum Mtitu na Nassoro Kibwana wanafafanua kwa kina kijiji chao ambavyo kwa sasa hakina miti baada ya watu kuvamia na kuchoma kuni huku wakieleza baada ya wavunaji haramu kuona hakuna miti tena wameondoka na kwenda Kimalamisale.

Wakati wananchi na viongozi wakielezea kwa kina kuhusu uharibifu wa misitu katika vijiji vyao, Kaimu Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki Mathew Ntilicha anaelezea kuwa wameendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa bodaboda.

“Tumekutana na viongozi wao mara kwa mara kwasababu wao ndio wasafirishaji mkaa.Machi 17 mwaka huu tumekutana nao ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kupitia kikao alichokifanya Mlandizi.

“Katika kikao chetu ikaonekana uelewa umeanza kuongezeka kuhusu sheria ya misitu inavyoeleza kwa anayetaka kufanya biashara ya mkaa.Kwa hiyo ni matumaini yetu jambo hili linakwenda kukaa vizuri na kumalizika.

“Kwa wenyeji wa maeneo ya Kibaha Vijijini katika vijiji vya Dutumi, Lukenge na vijiji vingine lakini hata kama unatokea Chalinze na maeneo mengine ya Kisarawe ukiangalia trend huko nyuma ya usafirishaji wa mkaa kwa kutumia bodaboda ulikuwa ni wa kiwango kikubwa.

“Kutokana na jitihada ambazo Serikali inazofanya ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na TFS tumepunguza tatizo hili kwa kiwango kikubwa sana. Sasa hivi ukipita barabarani huwezi kukutana na msururu mkubwa, utaona bodaboda mmoja mmoja,”anasema.

Pia anasisitiza TFS wanaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao wa mkaa ili warudi kwenye utaratibu ambao umeruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

“Ukiangalia operesheni tunayoifanya tumekutana na baadhi ya wafanyabiashara ambao kwa njia moja au nyingine wamekuwa si wepesi kutii maelekezo ya Serikali.

“Operesheni inayoendelea mpaka sasa hivi tuna kesi saba zenye watuhumiwa 45 na katika kesi hizo mbili ziko mahakamani na ziko kwenye hatua mbalimbali.Pia tuna kesi tano ziko polisi ambazo upelelezi unaendelea.

“Kwa hiyo sisi TFS haya matokeo tunayoyaona ya kupungua kwa bodaboda zilizokuwa zinafanya uvunaji holela ni mafanikio na tutaendelea kufanya doria na kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa mkaa hasa wa bodaboda wanarudi kwenye utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria.”

Kaimu Kamanda Ntilicha anasema TFS wameendelea kuwahamasisha wananchi na viongozi wa bodaboda na wamekubaliana kuwa na mkakati wa kufanya urejeshaji miti maeneo yaliyoharibiwa na uvunaji wa mkaa na bodaboda

“Tumeandaa program maalum ya upandaji miti maeneo yale kurudishia uoto ili kufanya mazao haya yaendelee kuwepo na yaendelee kusaidia kizazi cha sasa na vizazi vingine.

“Pia kama Serikali bado tunawakaribisha wafanyabiashara wa kutumia bodaboda kuna fursa nyingi ambazo TFS pia kupitia mfuko wetu wa misitu Tanzania huwa unatoa uwezeshaji kwa mtu mmoja mmoja, kikundi au taasisi

“Kinachotakiwa ni kuandika andiko linalohusiana na uhifadhi , ule mfuko wa misitu Tanzania huwa unatoa fedha , tunawakaribishia, na h ii itasaidia kuwatoa vijana kwenye biashara ya mkaa.

“Wanaweza kuandika miradi kuhusu upandaji miti , ufugaji nyuki wakapatiwa fedha kupitia mfuko wa misitu Tanzania na wakajikita kwenye shughuli ambazo zitawapatia kipato tofauti na uharibifu wa misitu wanayoifanya kwa kuvuna mkaa bila utaratibu.”

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here