Home LOCAL WAKAZI WA DODOMA WASHUKURU HUDUMA YA UPIMAJI MAGONJWA YA MOYO

WAKAZI WA DODOMA WASHUKURU HUDUMA YA UPIMAJI MAGONJWA YA MOYO

Wauguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wakiwapima wananchi   waliotembelea  banda la Taasisi hiyo shinikizo la damu na kiwango cha sukari mwilini wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya Baraza la Uuguzi  na Ukunga yanayoenda sambamba na maonesho ya siku tatu ya huduma zinazotolewa na wauguzi yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Adam Ndamayape akitoa elimu ya jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo kwa wananchi waliotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya Baraza la Uuguzi  na Ukunga yanayoenda sambamba na maonesho ya siku tatu ya huduma zinazotolewa na wauguzi yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga kutoka  Wizara ya Afya Ziada Selah akiwa katika picha ya pamoja na wauguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya Baraza la Uuguzi na Ukunga yanayoenda sambamba na maonesho ya siku tatu ya huduma zinazotolewa na wauguzi yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini humo.Kulia ni Mkurugenzi wa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya.

Picha na JKCI

Na: Mwandishi Maalum – Dodoma, 19/03/2023

Wakazi wa mkoa wa Dodoma wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma za upimaji wa viashiria vya magonjwa ya moyo pamoja na ushauri wa jinsi ya kuyaepuka magonjwa hayo bila malipo yoyote yale.

Huduma hiyo inatolewa katika maadhimisho ya miaka 70 ya baraza la uuguzi na ukunga yanayoenda sambamba na maonesho ya huduma zinazotolewa na wauguzi yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliofika katika banda la JKCI kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na kupata ushauri walisema elimu waliyoipata ni nzuri na imewasaidia kuwapa uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa ya moyo na jinsi ya kuepukana nayo.

ama Amina Ismail mkazi wa Makole alisema huduma aliyoipata kutoka kwa wauguzi ni nzuri na imemsaidia kufahamu shinikizo lake la juu na la chini la damu likoje kwani hii ni mara ya kwanza kupima kwa hiari kiwango cha sukari mwilini na shinikizo la juu la damu.

“Licha ya kufanya vipimo, nimepata elimu ya lishe bora ambayo imenifungua akili na kufahamu aina gani ya vyakula natakiwa kuvila ili vinisaidie kujenga mwili pamoja na kulinda moyo wangu ili uwe salama”,.

“Elimu ya lishe ni nzuri ninatoa ushauri kuwe na vipindi kama hivi redioni ili watu wengi zaidi waweze kupata ujumbe huu kwani wengi wetu wakiwemo watoto tunakunywa vinywaji vya kusindika zikiwemo soda na juisi bila kujua kuwa vinamadhara mwilini”, alisema Mama Amina.

Naye Emmanuel Jembe mkazi wa Chamwino alisema baada ya kutembelea katika banda hilo ameweza kupata elimu ya jinsi ya kutambua dalili za shambulio la moyo na madhara yake kwani hapo awali hakuwa anajua chochote kuhusu dalili za ugonjwa huo na  kusema kuwa hivi sasa ameweza kufahamu vizuri.

“Nimefahamu kuwa ugonjwa wa shambulio la moyo ni hatari kwani unaua na dalili za ugonjwa huu ni  maumivu ya kifua upande wa kushoto, kifua kubana kushindwa kupumua na wakati mwingine maumivu ya tumbo. Nitaenda kutoa elimu hii kwa wenzangu ili waonapo dalili hizi wawahi hospitali mapema” , alisema.

Akitoa elimu ya jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo  Afisa Uuguzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Adam Ndamayape alisema magonjwa ya moyo ni moja ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza na yanaweza kuepukika kwa kufuata mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kutotumia bidhaa za tumbaku, kutokunywa pombe kupitiliza, kula vyakula bora  na kufanya mazoezi.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here