Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Namibia zimesisitiza kuweka mikakati imara ya ushirikiano itakayoimarisha mfumo wa utendaji kazi kwa lengo la kukuza na kuendeleza Diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya nchi hizo pamoja na watu wake.
Msisitizo huo umetolewa katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Namibia unaofanyika Jijini Windhoek, Namibia kuanzia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023.
Akifungua mkutano huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tatu wa JCC kati ya Tanzania na Namibia kwa Ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Fatma Rajab ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kuweka mikakati imara ya ushirikiano na kukuza uchumi kati yake na Namibia ili kuuenzi ushirikiano wa kidugu na kihistoria uliopo baina ya nchi hizo.
Balozi Fatma ameongeza kuwa ushirikiano huo uliasisiwa tangu enzi za harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na waasisi wa mataifa hayo mawili, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Namibia, Hayati Dkt. Samuel Daniel Nujoma.
“Ni matumaini yangu mkutano huu utatuwezesha kusaini makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya anga ili kurahisisha uwepo wa safari za moja kwa moja baina ya nchi zetu na kuwezesha uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu” alisema Balozi Fatma.
Vilevile, Balozi Fatma alieleza kuwa kupitia fursa ya majadiliano ya mkutano huo Tanzania na Namibia zitafungua maeneo mapya ya ushirikiano ambapo, kwa upande wa Tanzania tayari imewasilisha mapendekezo ya makubaliano ya ushirikiano kwa Namibia katika sekta za ulinzi, biashara na uwekezaji, nishati na majadiliano ya kisiasa na diplomasia ambazo makubaliano yakikamilika zitarasimishwa na kusainiwa katika mkutano wa ngazi ya Mawaziri utaofanyika tarehe 10 Machi 2023 jijini Windhoek, Namibia.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Namibia ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza katika mkutano huo, Balozi Penda Naandi ameeleza kuwa takwimu za biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia bado ni ndogo, hivyo mkutano huo utaweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha ushirikiano huo unaleta maendeleo ya kiuchumi na kuinua maisha ya wananchi wa pande zote mbili.
“Nchi zetu zinashirikiana katika sekta za kiuchumi ambazo zinatuwezesha kuingia kwenye soko la ushindani katika Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na kuinua uchumi wa kikanda pamoja na kufikia malengo ya maendeleo endelevu kwa watu wake” alisema Balozi Naanda.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utapitia, kujadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa pili uliofanyika mwezi Desemba 2019 Jijini Dar es salaam, Tanzania.
Tanzania na Namibia zinashirikiana katika sekta za Diplomasia, Siasa, Ulinzi, Uvuvi na Rasiliamali za Bahari, Kilimo, Maji, Maendeleo ya Miji, Madini, Nishati, Biashara, Uwekezaji, Mazingira, Utalii na Maliasili, usafiri, Afya, Utamaduni na Elimu.