Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchemi Mramba amesema kuwa Kongamano la Kampuni za Gesi Afrika Mashariki linalofanyika Jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania ltaongeza uelewa na kukuza uwekezaji katika sekta ya Nishati hususani katika sekta ya gesi za Majumbani.
Mhandisi Mramba ameyasema hayo Machi 15, 2023 alipokuwa akifungua Kongamano hilo linalofanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa Wizara inaongoza mpango wa kuleta masuala ya Nishati safi ya kupikia nakwamba, mwaka uliopita 2022, Wizara hiyo iliendesha mkutano mkubwa uliobeba ajenda ya Nishati safi ya kupikia ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alitangaza kuunda mkakati wa Kitaifa wa Nishati safi ya kupikia 2033.
Ameeleza kuwa mpango huo utatimiza asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kaya za Watanzania ifikapo mwaka 2033 ambapo Nishati za kupikia kama vile LPG, Gesi Asilia (City Gas) na E-cooking zitaongeza tija katika utunzaji wa mazingra.
“Mambo makuu ya Sera ya Taifa ya Nishati ya 2015 ni pamoja na kuendeleza rasilimali za nishati za ndani ambazo ni chaguzi za gharama nafuu, kukuza bei ya nishati ya kiuchumi, kuboresha utegemezi wa nishati na usalama na kuongeza ufanisi wa nishati, kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi, kupunguza uharibifu wa misitu na kuendeleza rasilimali watu” ameeleza Mhandisi Mramba, na kuongeza kuwa.
“Natumai wakati wa mijadala katika hafla hii ya siku mbili mtapata fursa ya kujadili masuala ya mazingira na afya wakati wa kujadili sekta ya upishi ambayo katika nchi yetu ina sifa kubwa ya nishati asilia kama vile mkaa na kuni. Manufaa ya kutumia LPG kama nishati mbadala ya kupikia, Gharama, Uhamasishaji, masuala ya usalama kwa matumizi ya nyumbani ni miongoni mwa maeneo ambayo tunahitaji sana kupata uzoefu” ameongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Kampuni za Gesi nchini Tanzania, Araman Benoite ambaye pia ni Mkurugenzi wa Oryx Gas nchini amesena kuwa watanzania wamehamasishwa kuongeza nguvu katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuondokana na athari mbalimbali zikiwamo za mazingira, huku matumizi ya nishati safi ya kupikia yakitajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuendeleza uchumi kuanzia ngazi ya familia na taifa kwa ujumla.
Amesema kwamba bado kuna fursa ya uwepo wa soko kubwa la gesi ya majumbani kwani Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipambanua kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
“Kuna faida kubwa katika kutumia Nishati hii ambazo ni pamoja na kusaidia mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira, kuunga mkono jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutumia muda mchache katika shughuli za mapishi tofauti na pale endapo wangetumia nishati nyingine kupikia kama Kuni au mkaa” amesema Bw. Benoite.