NA: FARIDA MANGUBE, MICHUZI TV MOROGORO.
Wajumbe wa Dawati la jinsia Chuo kikuu Mzumbe kampasi kuu ya Morogoro wametakiwa kutunza siri na kutoa msaada unaostahili kwa walioathiriwa na Vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kujenga jamii iliyo bora.
Akizungumza wakati akifungua Dawati la jinsia chuo kikuu Mzumbe kampas kuu ya Morogoro kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Rebecca Nasemwa ambae amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo wa Morogoro Fatma Mwasa alisema kumekuwa na ongezeko la matukio yanayohusiana na unyanyasaji wa kijinsia na mashambulio ya aibu yanayohusisha wanafamilia na jamii kwa ujumla, hivyo kuzinduliwa kwa Dawati hilo maalumu liwe chachu ya kutokomeza ukatili wa jinsia chuoni hapo.
Alisema kuanzishwa kwa Dawati hilo ni moja ya hatua kubwa za kutimiza malengo ya serikali ya kupunguza na kumaliza kabisa ukatili wa kijinsia kwenye jamii hususani vyuoni.
“Mtu akinyanyaswa hata uwezo wake wa kufikiri unapungua maana atatumia muda mrefu kufikiria jinsi ya kujinasua badala ya kutumia muda huo kufikiria jambo lingine kwa ajili ya ustawi wa jamii.” Alisema Rebecca.
Aidha alikitaka chuo kikuu Mzumbe kupitia Dawati hilo kufanya tafiti na kuibua mambo ya ukatili yanayoendele kwenye vijiji vinavyozunguka Chuo hicho kwajili ya kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini.
Pia aliupongeza uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kujenga jengo maalumu kwa ajili ya Dawati la jisnia.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli aliwataka wanafunzi, walimu pamoja na watumishi wote ya Chuo Kikuu Mzumbe kutoa taarifa bila ya uwaga za unyanyasaji wa kijinsia kwenye Dawati hilo lililofunguliwa.
Naye Kaim Makamu Mkuu wa Chuo kikuu Mzumbe Prof.William Mwegoha alisema Dawati hilo litafanya kazi kwa kuzingatia muungozo wa Serikali.
Pia alitaja njia zitakazotumika kupata taarifa za unyanyasaji wa kijinsia ni pamoja na mlengwa kufika moja kwa moja kwenye ofisi za Dawati la jinsia, kupiga simu kupitia namba ya wazi ambayo mtu yeyote anaweza kupiga na kutoa taarifa zake na kutumia sanduku la maoni.
Kwa upande wao wanafunzi waliipongeza Serikali kupitua Chuo Kikuu Mzumbe kwa kufungua Dawati la jinsia chuoni hapo kwani litasaidia kupunguza unyanyasaji wa kijisnia unaofanywa na baadhi ya watu wasio na maadili.
Walisema ukatili na unyanyasaji wa kijinsia umekuwa ukisababisha wanafunzi wengi kutofikia malengo yao na wengine kuacha kabisa masomo.