Home BUSINESS MAZINGIRA WEZESHI KWA WAWEKEZAJI YAFIKISHA VIWANDA 1,522 PWANI

MAZINGIRA WEZESHI KWA WAWEKEZAJI YAFIKISHA VIWANDA 1,522 PWANI


Na: Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa inaweka mazingira wezeshi ambayo yanawawezesha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wote wa taasisi binafsi kuweza kufanya biashara na uwekezaji katika Mkoa wa Pwani.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Pwani kutoka Idara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Rehema Akida ameyasema hayo hivi karibuni mkoani Pwani wakati akizungumza na Maafisa Habari wa Idara ya Habari – MAELEZO kuhusu uwekezaji wa viwanda uliopo katika mkoa huo.

“Vitu vinavyovutia wawekezaji mkoani Pwani ni kuwa karibu na masoko likiwemo soko kuu la Dar es Salaam, miundombinu ya barabara ya kufikia masoko ya ndani, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika Mashariki, uwepo wa miundombinu katika maeneo ya uwekezaji pamoja na uwepo wa kituo cha huduma za pamoja kinachowasaidia wawekezaji kupata huduma zinazohitajika kiurahisi.” Alisema Rehema Akida.

Amesema kuwa, mkoa huo umekuwa na maendeleo makubwa katika sekta ya viwanda ambapo kwa mwaka 2021, mkoa ulikuwa na viwanda 1,453 na katika kipindi cha miaka miwili mkoa umeweza kuwa na viwanda 1,522 ongezeko la viwanda 69 vikiwemo vikubwa 27 na vidogo 94 na vingine vingi vidogo.

Katibu Tawala Msaidizi ameongeza kuwa, kati ya viwanda vilivyokuwepo mwaka 2021, jumla ya viwanda saba vimeweza kupiga hatua ya kimaendeleo kutoka viwanda vya kati na kuwa viwanda vikubwa hiyo yote ikisababishwa na uwepo wa mazingira wezeshi ya kufanyia biashara.

Ameeleza kuwa, mkoa una viwanda vya aina mbalimbali vikiwemo viwanda vikubwa tisa (9) vya kutengeneza na kuunganisha magari, viwanda 17 vya kuchakata mazao mbalimbali ya kilimo, kiwanda kikubwa cha sukari cha Bagamoyo, viwanda vinavyohusika na utengenezaji wa nguzo za umeme za zege pamoja na viwanda 14 vya kuchakata mazao ya mifugo na ngozi.

Vile vile Mkoa wa Pwani umetenga ardhi kwa ajili ya maeneo ya viwanda ambapo kwa sasa mkoa una jumla ya kongani 23 za ujenzi wa viwanda ambapo tatu kati ya hizo zimeanzishwa mwaka 2022, ikiwemo Kongani ya Kisasa ya Viwanda ya Kamala na SinoTan zitakazojumuisha viwanda mbalimbali.

Aidha, uwepo wa viwanda mkoani humo umekuwa na manufaa kwa kutoa ajira hivyo kukuza kipato na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja ambapo kwa miaka miwili hii, jumla ya ajira 17,659 za moja kwa moja na 50,000 zisizo za moja kwa moja zilipatikana, kuongezeka kwa mchango mkubwa wa viwanda katika Pato la Taifa ambapo mkoa umeshika namba tatu kwa mwaka 2022 katika uchangiaji Pato hilo. Aidha, mkoa umeshika nafasi ya saba katika uchangiaji wa Pato la Taifa katika madini kwa sababu ya uwepo wa viwanda vinavyotumia madini ujenzi.

Mkoa wa Pwani ni eneo zuri na sahihi kwa uwekezaji wa aina yoyote na hakuna changamoto katika upatikanaji wa huduma, pia usalama ni wa hali ya juu kwani hakuna kesi ya aina yoyote iliyowahi kutokea ambayo inasababisha uvunjifu wa amani kwa wawekezaji wetu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here