Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Michael Battle ameipongeza Tanzania kwa uwazi na utoaji wa haraka wa Taarifa kwa umma kuhusiana na ugonjwa wa Marburg mkoani Kagera.
Ameyasema hayo leo tarehe 23 Machi,2023 jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye ofisi za wizara.
“Tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa wa wazi hasa katika utoaji wa taarifa za magonjwa ya mlipuko kwa haraka ikiwemo hii ya ugonjwa wa Murburg” Hakika mmeonyesha uongozi bora kwa dunia kuhusu usalama wa Afya kwa watanzania na dunia”. Alisema Balozi Battle.
Ameendelea kusema kuwa ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris kuitembelea Tanzania itawakutanisha Wanawake wawili wenye ushawishi Duniani. Na hivyo ni jambo la kupongezwa.
Naye, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Tanzania itaendelea kutimiza wajibu wake kwa kuzingatia Kanuni za Kimataifa za Afya kwa kutoa taarifa mapema ili kuweza kuwalinda wananchi wake pamoja na usalama wa afya wa kimataifa.