Home LOCAL MAKAMU WA RAIS AFANYA MAZUNGUMZO NA KAMATI YA BUNGE PIC

MAKAMU WA RAIS AFANYA MAZUNGUMZO NA KAMATI YA BUNGE PIC

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Mwenyekiti kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Jerry Silaa wakati alipowasili katika eneo la Misunzu Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma kukagua Ujenzi wa Barabara ya Kabingo-Kasulu- Manyovu leo tarehe 22 Machi 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na wajumbe wa  kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Jerry Silaa wakati alipowasili katika eneo la Misunzu Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma kukagua Ujenzi wa Barabara ya Kabingo-Kasulu- Manyovu leo tarehe 22 Machi 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema kukamilika kwa ujenzi barabara ya Kabingo- Kasulu-Manyovu kutafungua mkoa wa Kigoma kiuchumi na biashara baina ya mkoa huo na mikoa mingine pamoja na nchi jirani.

Makamu wa Rais amesema hayo akiwa eneo la Busunzu wilayani Kibondo mkoani Kigoma leo tarehe 22 Machi 2023 wakati akizungumza na kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma inayokagua maendeleo ya  ujenzi wa miradi mbalimbali mkoani humo. 

Amesema barabara hiyo ni mkombozi wa mkoa wa Kigoma kutokana na wananchi wa mkoa huo kufanya biashara kwa wingi na mikoa ya Shinyanga na Mwanza pamoja na nchi ya Burundi hivyo kukamilika kwake kutachochea maendeleo ya mkoa huo na nchi kwa ujumla. Aidha Makamu wa Rais amesema lengo la serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona mkoa wa Kigoma unapata maendeleo kwa haraka kadiri inavyowezekana.

Makamu wa Rais ameagiza Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) kumsimamia mkandarasi kikamilifu ili kuhakikisha barabara hiyo ya kilometa 260.6 inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili. Aidha ametoa rai kwa serikali ya mkoa wa Kigoma kusimamia vema miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.

Kwa Upande wake Mwenyekiti kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Jerry Silaa ameipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa na wenye tija katika mkoa huo ambao utaleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi. Amesema kwa sasa wameshuhudia mkoa huo ukipiga hatua za maendeleo katika sekta za nishati na miundombinu kama reli na barabara. 

Mwenyekiti huyo amesema uwekezaji wa mitaji ya umma umefanyika kwa usahihi na tayari tija imeanza kuonekana. Ametoa wito kwa wananchi wa Kigoma kuendelea kuiunga mkono serikali kwani kazi kubwa inafanyika na dhana ya kazi iendelee inaonekana kwa vitendo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here