Home LOCAL MAKAMU WA RAIS AKIHUTUBIA MKUTANO WA UN DOHA QATAR

MAKAMU WA RAIS AKIHUTUBIA MKUTANO WA UN DOHA QATAR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akihutubia katika Mkutano wa Tano  wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea za Kipato cha Chini unaofanyika Doha Nchini Qatar. Tarehe 05 Machi 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa nchi na serikali kutoka katika mataifa mbalimbali duniani pamoja na viongozi wa taasisi za kimataifa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano  wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea za Kipato cha Chini unaofanyika Doha Nchini Qatar. Tarehe 05 Machi 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Nchi Zinazoendelea za Kipato cha Chini (LDCs) kuhakikisha zinafanya maboresho ya kina ya kisera,kisheria na kitaasisi ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kukuza sekta binafsi, kuongeza uwekezaji pamoja na  kuleta mageuzi ya kiteknolojia.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 05 Machi 2023 wakati akihutubia Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea za Kipato cha Chini unaofanyika Doha Nchini Qatar.  Ameongeza kwamba ili kufikia na kutimiza Maazimio ya Doha ni muhimu mataifa yanayoendelea ya kipato cha chini kuwekeza zaidi katika rasilimali watu ya vijana na wanawake pamoja kuhakikisha zinaweka mkazo katika elimu bora, ujuzi, huduma za afya na miundombinu ikiwemo nishati, reli, bandari na tehama.

Pia Dkt. Mpango amesisitiza  kuimarisha  ushirikiano baina ya nchi na nchi ,kikanda  na kimataifa pamoja na kuhakikisha  nchi hizo zanapata fedha za kutosha za masharti nafuu kutoka katika Taasisi za Fedha za kimataifa na washirika wa maendeleo.

Makamu wa Rais ameeleza  changamoto mpya zilizoikumba dunia ikiwamo janga la UVIKO, athari za mabadiliko ya tabia nchi na migogoro ya kimataifa ambazo zimezifanya nchi za kipato cha chini kupiga hatua hafifu katika utekelezaji wa maazimio ya Mkutano kama huo uliofanyika jijini Instambul Uturuki miaka kumi iliyopita.

Akitoa Uzoefu wa Tanzania kama nchi ya Uchumi wa Kati wa chini  Makamu wa Rais ameeleza  jitihada na mafanikio yaliofikiwa  katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu wake ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwa nchi inayokua kiuchumi kwa kasi kusini mwa jangwa la sahara, umri wa kuishi kuongezeka  kutoka miaka 60 mwaka 2010 hadi miaka 67.2 mwaka 2022 pamoja na  idadi ya watoto chini ya miaka 5 ambao wana utapiamlo kupungua  kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 30 mwaka 2022

Makamu wa Rais ameongeza kwamba kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka 5 kimepungua  kutoka vifo 81 mwaka 2010 hadi vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2022, kiwango cha vifo vya uzazi kilipungua kutoka vifo 432 mwaka 2015 hadi 250 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2021; na maambukizi ya malaria kwa watoto wenye umri wa miezi 6-56 kimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2007/08 hadi asilimia 8 mwaka 2021/22.

Katika sekta ya elimu amesema, kiwango cha uandikishaji katika ngazi ya shule ya msingi kimeongezeka kutoka asilimia 85 mwaka 2015 hadi asilimia 97 mwaka 2021 kutokana na serikali kutoa elimu bila malipo. Pia amesema  uboreshaji na  ubunifu wa fedha za kidijitali umeongeza  matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu nchini kote.

Makamu wa Rais amesema kupitia hatua ilizopiga nchi ya Tanzania katika maendeleo ni wazi muda muafaka wa taifa hilo kuondolewa katika kundi la nchi za kipato cha chini umekaribia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here