Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeonesha kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo Kame nchini (LDSF) katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Hayo yamejiri leo Machi 16, 2023 wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua ujenzi wa jengo la kukusanyia mazao ya nyuki, banda la kuku, shamba darasa na uchimbaji wa visima chini ya mradi huo unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza wakati wa ziara Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswaga amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa usimamizi na ufuatiliaji wa mradi huo akisema umelinana na thamani ya fedha zilizotolewa.
Mhe. Kiswaga amesema kuwa mradi wa ufugaji wa nyuki katika Kijiji cha Sigili wlayani hapo ni wa mfano kwani unasaidia kuhifadhi na kulinda mazingira kupitia misitu ambayo mizinga imetundikwa.
Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kupanda miti na kuitunza ili kuweza kukabiliana na athari hasa za kimazingira ambazo zinasababisha ukosefu wa mvu katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ndugu zangu sisi Bunge kama Chombo kinachosimamia maendeleo ya wananchi tumejifunza mambo makubwa hapa Nzega kwenye mradi huu na tutautumia kama mfano kuwaelemisha katika maeneo mengine ili nao wajifunze,“ amesema Mhe.Kiswaga.
Wajumbe wa kamati hiyo pamoja na kutoa pongezi pia wametoa ushauri kuwa miradi kama hiyo itekelezwe katika maeneo mengine ya nchi wananchi wanufaike nayo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kwa kutembelea mradi huo na kuona namna Serikali inavyohakikisha wananchi wake wananufaika na miradi ya mazingira.
Pia, ameahidi kuwa Ofisi itaendelea kuisimamia vyema miradi hii ili iendelee kuleta matokeo mazuri kwa wananchi hasa katika eneo la kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi linalolikabili taifa letu.
“Niwapongeze Halmashauri ya Nzega kupitia kwa Mkurugenzi wake na wataalamu wote kwa kufanya vizuri katika mradi huu na sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tutahakikisha tunausimamia vizuri mradi huu,“ amesema.
Mradi wa LDFS unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega (Tabora), Magu (Mwanza), Mkalama (Singida), Kondoa (Dodoma) na Micheweni (Pemba).