Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa fadhili, kwa kutupatia afya njema na kutuwezesha kufika hapa Dodoma kwa ajili ya mafunzo ya Wakuu wa Wilaya. Asnateni sana viongozi wetu wa dini kwa kuweka mkutano huu mbele ya Mungu. Aidha, napenda kutumia nafasi hii kukupongeza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule kwa kukubali kuwa mwenyeji wa semina hii ya kuwajenga na kuwafunda Wakuu wetu wa Wilaya nchini.
Kipekee kabisa, napenda kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi Mheshimiwa Angellah Kairuki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na wale wote walioshiriki kuandaa vizuri semina hii muhimu sana. Aidha, nawashukuru pia Taasisi ya UONGOZI kwa kukubali kuja kutoa mada katika mafunzo haya na kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo kwa viongozi wetu wa ngazi mbalimbali hapa nchini ili kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa weledi na tija kubwa zaidi.
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya mliopo hapa
Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa kwa kuteuliwa kwenu (wapya kabisa na wale mnaoendelea na nafasi zenu). Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonesha imani kubwa sana juu yenu. Hivyo, hamna budi kuitendea haki dhamana kubwa mliyopewa kwa kutekeleza majukumu yenu kwa weledi, uzalendo na kwa kujituma (working beyond the call of duty = exceed usual limits in quality and quantity). Aidha, Mheshimiwa Rais amenituma nifungue mafunzo haya kwa niaba yake na niwaeleze kuwa ameruhusu mafunzo haya yafanyike, ili muwezeshwe
kuwatumikiwa wananchi ipasavyo katika misingi ya sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Aidha Mheshimiwa Rais ameniagiza niwasisitize kusoma Miongozo yenu ya kazi kwa umakini ili muweze kusimama vizuri kwenye nafasi zenu na kutekeleza majukumu yenu kwa weledi mkubwa. Aidha, Mheshimiwa Rais anawakumbusha kuendelea kusikiliza na kutatua shida za wananchi, kukemea mabaya katika jamii na yale yanayopunguza tija au kukwamisha maendeleo ya Taifa. Wakuu wa Wilaya mnapaswa kuwa wahabarishaji mahiri (good communicators) wa mipango ya maendeleo katika Wilaya na kuhabarisha wananchi mazuri yanayotekelezwa na Serikali unayoiongoza, na kwa kurejea ahadi zilizomo katika Ilani ya Chama Tawala.
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.
Semina kama hii ni muhimu sana kwa kuwa inatupatia fursa ya kujitafakari, kujitathmini, kujipanga upya na ikibidi, kujirekebisha. Nafahamu kwamba baadhi yenu mambo mtakayojifunza yatakuwa ni nyongeza ya yale mnayoyafahamu, na
kwa wengine yanaweza kuwa mageni. Vyovyote vile, kwa ujumla wake mafunzo haya yatawapa stadi za kazi, ujuzi na mwelekeo katika utendaji wenu wa kazi.
Mkumbuke kuwa mmepewa dhamana kubwa ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 na usimamizi wa sera pamoja na shughuli nyingine za Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan Ibara ya 34(4)1. Hivyo imani yetu ni kuwa, baada ya mafunzo haya mtakuwa mahiri na tayari kusimamia shughuli zote za Serikali katika Wilaya zenu.
Tumesikia hapa mada zitakazowasilishwa. Mada zote ni muhimu sana katika utendaji wenu wa kila siku. Hata hivyo, napenda kutumia nafasi hii kutoa msisitizo kwenye maeneo machache kama ifuatavyo:
Kwanza, ni kwenye mada inayohusu Muundo wa Serikali Kuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Majukumu na Mipaka ya Kazi, naamini katika eneo hili mtaeleweshwa majukumu ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na namna gani zinafanya kazi pamoja katika kuwatumikia watanzania bila kuingiliana na kuleta migogoro. Bila shaka majukumu ya msingi ya Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Miji na Majiji na pengine hata Wabunge yatafafanuliwa vizuri. Hivyo, ni matarajio yetu kuwa mtazingatia kikamilifu mipaka yenu ya madaraka, mtashirikiana kuchochea maendeleo katika Wilaya na kwamba hatua mtakazozichukua katika Uongozi na utendaji wenu zitazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo bila kuathiri majukumu ya wengine.
Pili, ni kuhusu Utunzaji wa Siri za Serikali. Jambo hili ni muhimu sana hususani katika kipindi hiki cha utandawazi na matumizi ya mitandao ya kijamii. Yawapasa mzingatie kuwa SIRI ndio uhai wa Serikali. Hivyo, ni lazima kudhibiti uvujaji wa siri za Serikali. Epukeni kabisa kutumia mitandao ya kijamii kama WhatsApp, ama email binafsi kutuma nyaraka za Serikali. Aidha, kwenye hili pia watoa mada hakikisheni mnatoa msisitizo kuhusu matumizi ya Walinzi binafsi (bodyguards) na Waandishi wa Habari binafsi katika Ofisi za Umma. Zipo taratibu za kufuata endapo itabainika Kiongozi anahitaji kupatiwa wasaidizi wa aina hii. Zingatieni taratibu zilizopo na si vinginevyo. Kiongozi asipofuata utaratibu unaotakiwa kuwapata watumishi hao na kuamua kujitafutia mwenyewe wakati mwingine inakuwa si salama kwa kiongozi mwenyewe na hata siri za Serikali. Vilevile, kuweni makini maneno mnayoyazungumza (kupiga story) na
1 34(4) Bila kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, madaraka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatatekelezwa ama na Rais mwenyewe moja kwa moja au kwa kukasimu madaraka hayo kwa watu wengine wenye madaraka katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
wasaidizi wenu hususan madereva na watu wengine mnapokuwa nje ya ofisi/sehemu za starehe ili kuepuka kutoa siri za Serikali.
Tatu, ni kuhusu Ulinzi na Usalama. Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, hili ni jukumu lenu la kwanza na ninyi ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi wa Usalama katika Wilaya zenu. Hivyo, hamna budi kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinakuwepo kwenye maeneo yenu wakati wote. Hakuna maendeleo bila Amani na usalama wa raia na mali zao. Kuweni wepesi na wabunifu katika kutatua migogoro kwenye Wilaya zenu hususan migogoro ya ardhi na mipaka, migogoro baina ya wakulima na wafugaji na baina ya wafugaji au wakulima na hifadhi. Vilevile mdhibiti uhasama ndani ya jamii au na vyombo vya dola, mauaji n.k. mkawe walinzi wa haki za watu wote hususani wanawake na watoto. Tumieni busara katika kusuluhisha migogoro iliyopo katika maeneo yenu kwa kuzingatia Sheria za Nchi, Kanuni na Taratibu. Simamieni isiibuke migogoro mipya ya wakulima na wafugaji; au ya matumizi mbalimbali ya rasilimali. Natoa rai kwenu, acheni kukaa maofisini. Kila Mkuu wa Wilaya afanye jitihada kuijua vizuri Wilaya aliyokabidhiwa ikiwemo fursa zilizopo, mila na desturi na changamoto pia. Ninyi ndio macho yetu katika Wilaya mlizokabidhiwa. Mkifanya kazi yenu inavyopaswa, malalamiko ya wananchi kwa Serikali yatapungua au kuisha kabisa. Hakikisheni mnajenga mahusiano mazuri na kushirikiana na wananchi, viongozi wengine (wa kimila, dini) pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye maeneo yenu.
Mada nyingine ambayo ningependa kuiwekea mkazo ni ile ya Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo na matumizi sahihi ya Utaratibu wa “Force Account.” Kumbukeni kuwa moja ya majukumu ya msingi ya kila Mkuu wa Wilaya ni kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa sera, mipango, ilani na shughuli zote za maendeleo katika eneo lake la utawala. Serikali ya awamu ya sita imekuwa inapeleka fedha nyingi sana katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Lakini, ni ukweli ulio wazi kwamba kumekuwa na wizi na ubadhirifu mkubwa wa fedha za miradi ya maendeleo na kupelekea wananchi kukosa huduma na baadhi ya miradi hiyo kukosa thamani halisi ya fedha. Hivyo, hakikisheni mnaielewa vizuri mada hii ili muweze kusimamia miradi na hasa matumizi sahihi ya utaratibu wa Force Account.
Ndugu Viongozi,
Kwakuwa hii ni mara yangu ya kwanza kukutana nanyi kwa pamoja tangu mlipoteuliwa, napenda kutoa maelekezo yafuatayo kwenu:
Jambo la kwanza ni kuhusu Utawala Bora. Ninyi Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya ni kiungo muhimu sana ndani ya Serikali kwani ndio macho na masikio ya
Serikali katika kutambua na kushughulikia changamoto za wananchi, kwa kuwa mko karibu zaidi na wananchi. Kwa kutambua hilo, kahakikisheni kila Mwenyekiti wa Kitongoji na Kijiji, kwa uratibu wa Afisa Mtendaji, anatimiza wajibu wake wa kuitisha mikutano ya Kisheria inayohusu mipango ya maendeleo pamoja na kuwapatia mrejesho wananchi kwa kuwasomea taarifa za mapato na matumizi. Hakikisheni mnajiwekea utaratibu wa kusikiliza kero za Wananchi na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati. Nendeni mkawe msaada kwao na sio kikwazo au kero.
Nyinyi ni Watumishi wa Wananchi na sio mabwana.
Aidha, dumisheni uhusiano mwema baina yenu na watumishi walio chini yenu, kwa kuzingatia kuwa kila mtumishi anao mchango katika kuboresha utendaji2. Vilevile, epukeni migogoro ya kiutendaji na viongozi wenzenu hususan Wakurugenzi wa Halmashauri. Hakikisheni mnazingatia mipaka yenu ya madaraka na kazi, na kwamba hatua mtakazozichukua katika utendaji wenu wa kazi zinazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utendaji kazi katika Utumishi wa Umma na Serikali kwa ujumla. Kadhalika, dumisheni uhusiano mzuri wa kazi na viongozi wengine ndani ya mihimili yote mitatu (Serikali, Bunge, Mahakama) pamoja na Viongozi wa Chama na hata wale wa Kimila na Taasisi za Dini. Kafanyeni kazi kwa pamoja na kushirikiana. Sote tunajenga nyumba moja! Na hapa nisisitize kwamba ninyi ni Makamisaa wa Chama chetu, hivyo mtoe ushirikiano wa kutosha kwa viongozi na watendaji wa Chama chetu katika maeneo yenu. Hao ndio wenye duka!
Jambo la Pili ni Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi. Miongoni mwa vigezo tunavyovitumia kupima tija ya utendaji kwenye Halmashauri ni uwezo wa kukamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa na kwa viwango vilivyokusudiwa hasa kwa miradi ambayo imepelekewa fedha. Napenda niwaambie waziwazi kuwa, hatutaendelea kuvumilia uzembe, ubadhirifu na kukosa uadilifu na uaminifu. Kasimamieni tija ya utendaji katika maeneo yenu na kutumia elimu mtakayoipata hapa ya usimamizi wa miradi, kuondoa dosari za kiutendaji zinazoweza kujitokeza.
Jambo la tatu, ninalowataka mkalisimamie, ni suala la kuongeza ukusanyaji wa Mapato ya Serikali na kudhibiti uvujaji wa mapato hayo. Mkakati wetu wa kujitegemea kibajeti unategemea uwezo wetu wa kukusanya mapato ya ndani. Hivyo, mkasimamie na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri zenu na kudhibiti matumizi yasiyo na tija. Aidha, hakikisheni
2 Inawezekana baadhi yenu mnajua kitabu cha Simon Sinek kinaitwa “Leaders Eat Last”! ambaye alibaini utaratibu wa viongozi wa Jeshi la Wanamaji la Marekani kugawiwa chakula baada ya askari wote wa vyeo vya chini kupata chakula. Msingi wake ni kuwa gharama halisi ya uongozi ni utayari wa kutanguliza mahitaji ya wengine kabla ya mahitaji yako binafsi. Viongozi mashuhuri ni wale ambao wanawajali kweli kweli watu ambao wamepewa heshima kuwaongoza.
mnaziba mianya yote inayosababisha fedha nyingi za Serikali kupotea. Mtakaporejea kwenye Wilaya zenu hakikisheni malipo yanafanyika kielektroniki na fedha zinapelekwa benki kwa wakati. Na katika hili niseme wazi, yeyote atakayegundulika kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu wa fedha za Serikali,
hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria na taratibu hata kama utakuwa katika Wilaya au wadhifa tofauti na sasa.
Jambo la nne, ni kuhusu usimamizi wa Miradi ya Maendeleo. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri Kairuki katika ziara zake akisisitiza kuhusu kuhakikisha Miradi ya Maendeleo inayobuniwa na Halmashauri zenu iwe ni ile yenye tija na manufaa kwa wananchi, na amekuwa akisisitiza kuhakikisha asilimia 40 au 60 ya fedha inayotengwa kutoka katika mapato ya ndani ya Halmashauri zenu zipelekwe kwa wakati na kusimamiwa. Kwenye hili napenda kuwakumbusha kuzingatia ubora wa Miradi na kuhakikisha inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa. Haikubaliki kuona Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru au Kiongozi mwingine wa juu anapofika na kuanza kutoa kasoro za Mradi ambao wewe Mkuu wa Wilaya kila siku upo hapo na ndio eneo lako la kazi lakini na wewe unazishangaa kasoro hizo!. Hii si sawa hata kidogo. Zingatia kuwa kila Mradi unaotekelezwa katika eneo lako unapaswa kuufuatilia kwa kila hatua kuhakikisha Mradi huo unakamilika kwa viwango vilivyokubaliwa.
Jambo la tano, ni usimamizi wa Nidhamu, Maadili na Uwajibikaji. Simamieni maadili mema nidhamu kazini na uwajibikaji wa Watumishi kwa wananchi. Msiende kuwa Miungu watu! Nendeni mkatende haki kwa wananchi na watumishi walio chini yenu. Wahudumieni wananchi kwa staha, sikilizeni kero zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati. Ninyi kama Viongozi mnapaswa kuongoza kwa mfano na kuweni makini wakati wote mnapozungumza na Umma, hakikisheni mnatumia lugha fasaha na nzuri. Epukeni kutoa lugha ya matusi. Aidha, mienendo yenu na muonekano wenu mbele ya jamii uwe ni wa mfano. Mienendo isiyofaa kama ulevi, ufuska, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya madaraka yenu, ufisadi, rushwa n.k. haiendani kabisa na dhamana au heshima ya Mkuu wa Wilaya. Ukiwa na sifa hizo mbaya, achia ngazi kabla ya kutenguliwa kwa aibu. Mkuu wa Wilaya tunayemtarajia ni yule anayetenda haki, mwaminifu/mnyoofu, mwadilifu, mwenye tabia njema na mchapakazi. Hali kadhalika, niwakumbushe kuwa ninyi mmeshika mpini wa fyekeo la Serikali. Wazembe, wezi na wabadhirifu kwenye Halmashauri zetu lazima wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Serikali. Kila Kiongozi lazima awe makini muda wote. Ninaamini pia wakuu wa wilaya ni walezi na walinzi wa maadili, mila , desturi na utamaduni wa mtanzania hivyo hamtafumbia macho mmomonyoko wa maadili.
Jambo la Sita, ni suala la usafi na Uhifadhi wa Mazingira. Dunia yetu kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bionuwai, pamoja na uchafuzi wa mazingira. Ili kuwa na maendeleo endelevu, zingatieni na kuimarisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira pamoja na usafi katika maeneo yenu. Toeni hamasa kwa wananchi na hasa vijana ili wawe mstari wa mbele katika shughuli za uhifadhi ikiwemo kupanda miti (ya matunda, dawa, mbao, ufugaji nyuki) na , kusimamia mipango miji usafi wa maeneo yenu. Simamieni suala la uhifadhi wa vyanzo vya maji na matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa. Ni hivi karibuni, Mheshimiwa Rais katika Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya kupikia (Clean Cooking Conference) alisisitiza hili, ili Taifa letu liweze kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia na kufikia asilimia 80 kufikia 2032. Tekelezeni agizo hili kwa njia shirikishi, kupitia taasisi husika kwa mfano REA, SIDO na taasisi zisizo za kiserikali, ikiwemo sekta binafsi.
Jambo la Saba, jengeni tabia ya kujiongezea maarifa kwa namna mbalimbali ikiwemo matumizi ya mtandao (internet), kusoma vitabu, taarifa mbambali na takwimu kuhusu viashiria mbalimbali vya maendeleo na pia hata kupata busara kutoka kwa wazee wetu mbalimbali ambao wapita katika nyadhifa mbalimbali za uongozi. Hii ni karne ya sayansi na teknolojia, pateni fursa ya kujiongezea
maarifa ili muwe wabunifu na kuepuka kufanya mambo kwa mazoea.
Mwisho, nimeelezwa pia kutakuwa na siku maalum ambayo mtakutana na Mawaziri wa Sekta za Elimu, Afya, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii, Ardhi na Viwanda na Biashara na kuelezwa vipaumbele vya Wizara hizo. Sekta hizo ni za kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Sita. Hivyo, hakikisheni mnazielewa Wilaya zenu, mnakuwa wabunifu na muende mkasimamie kikamilifu vipaumbele vya sekta hizo katika Wilaya na Halmashauri zenu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
Aidha, kaitumieni vizuri Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika ngazi ya Wilaya. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji nayo ijielekeze kuwajengea Halmashauri uwezo wa kitaalam na kuwapatia vitendea kazi ili wasaidie kuhamasisha uwekezaji katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwasihi sana mtumie muda wa mafunzo haya kusikiliza, kuuliza na kujadiliana kwa uwazi. Aidha, msisite kuleta mapendekezo yenu Serikalini endapo yapo masuala mahsusi ya Kisera au Kisheria ambayo mnadhani endapo yakirekebishwa, uongozi na utendaji wenu wilayani utaimarika zaidi.
Mwisho kabisa, nawashukuru wote kwa kufika kwenye mafunzo haya na ninawapongeza sana kwa mara nyingine tena kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais. Aidha, napenda kuungana na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwatakia kila la kheri katika majukumu yenu. Mwenyezi Mungu awatangulie, awaongoze na kuwapa afya njema ili muweze kuwatumikia Watanzania kuwaletea maendeleo na kuacha alama chanya ya kukumbukwa. OR Tamisemi nimefurahi kuwa mafunzo kwa MaDCs na MaRCs yatakua endelevu.
Baada ya kusema haya, napenda sasa kutamka kuwa Mafunzo kwa Wakuu wa Wilaya wote Nchini 2023 sasa yamefunguliwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza,