Home Uncategorized DKT.DIMWA- AWAWEKA KIKAANGONI KAMPUNI YA ZABUNI YA UNUNUZI WA VIFAA TIBA.

DKT.DIMWA- AWAWEKA KIKAANGONI KAMPUNI YA ZABUNI YA UNUNUZI WA VIFAA TIBA.

NA: IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’,amewataka viongozi na watendaji wa serikalini kuchunguza na kufuatilia kwa kina kampuni zinazoshinda zabuni za usambazaji na ununuzi wa vifaa serikalini kama zina uwezo wa kutoa huduma hiyo kwa wakati ulioainishwa katika mikataba ya kisheria.

Rai hiyo ameitoa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, mara baada ya    kukagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Kivunge Unguja.

Amesema kuna baadhi ya makampuni yamekuwa na tabia za ubabaishaji katika kutekeleza makubaliano ya mikataba ya kisheria walioisaini baina yao na serikali hali inayosababisha kuchelewesha vifaa mbali mbali na kupelekea kukwama kwa miradi ya kutoa huduma kwa wananchi.

Dkt.Dimwa, ameweka wazi msimamo wake kuwa CCM haitowavumilia watendaji,viongozi wa Chama na Serikali pamoja na makampuni wanaokwamisha utekelezwaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Alisema wananchi ndio waliotoa ridhaa kwa Chama kushinda hivyo hawatakiwi kuteseka na kudhalilika kutokana na uzembe wa watu wachache wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao kwa wakati.

“Kuna miradi mbali mbali nchini imekwama kutokana na makampuni yanayopewa zabuni kutotekeleza wajibu wao na wengine wanatapeli fedha za umma na kutoweka kabisa, makampuni ya aina hiyo tutayashitaki kwa mujibu wa sharia.

Wananchi waliotupa ridhaa ya kuongoza dola hawawezi kuteseka,kulalamika na kukosa huduma muhimu wakati serikali yetu ipo na chama chao kipo.”, alitoa msimamo huo Dimwa.

Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, aliwapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi kwa juhudi zao za kutekeleza ilani ya CCM kwa kasi kubwa.

Maelekezo hayo Dkt.Dimwa, aliyatoa mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kaskazini ‘A’ iliyopo Kivunge kukuta ujenzi wake umekamilika lakini haina vifaa tiba.

Naye Mkurugenzi tiba Wizara ya Afya Zanzibar Dk.Marijani Msafiri, alisema ujenzi wa hospitali hiyo umekamilika licha ya kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa tiba vilivyocheleweshwa na kampuni iliyopewa zabuni ya kukunua vifaa hivyo.

Alisema tayari suala hilo amekabidhiwa mwanasheria wa wizara hiyo afuatilie na kutoa mapendekezo ya kisheria kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa kumaliza tatizo hilo ili wananchi wa wilaya hiyo na vijiji jirani wapate huduma za afya.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Siasa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo Ayoub Mohamed Mahmoud,alisema serikali imetekeleza kwa ufanisi miradi mbali mbali ya maendeleo katika sekta za afya,elimu,utalii,uvuvi,ufugaji,barabara na kuongeza miundombinu ya maji safi na salama.

RC Ayoub, aliwasihi wananchi kuendelea kuiamini serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi kuwa ina dhamira ya kumaliza changamoto mbali mbali ili kila mtu aishi maisha bora.

Mkuu wa Mkoa huyo Ayoub, alisema ibara ya 148 (d) imeelekeza uimarishaji wa hospitali ya Kivunge ili itoe huduma katika ngazi ya Mkoa.

Mapema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Ndg.Idd Ali Ame,alimpongeza Naibu Katibu Mkuu huyo kwa maamuzi yake ya kutembelea mradi huo wa kimkakati wenye manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa huo.

Alisema miradi ya maendeleo inaposhindwa kukamilika kwa wakati inasababisha wananchi kukilaumu Chama Cha Mapinduzi kinachosimamia utekelezaji wa ilani ya CCM.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here