Home LOCAL Cde.MBETO- ATAKA MIRADI YA KUACHA ALAMA ZA MAENDELEO

Cde.MBETO- ATAKA MIRADI YA KUACHA ALAMA ZA MAENDELEO

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg.Khamis Mbeto Khamis,akikabidhi jezi kwa ajili ya mazoezi ya mpira wa miguu kwa viongozi wa timu za Jimbo la Chaani zilizotolewa na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe.Nadir Abdullatif  ikiwa ni sehemu ya kuimarisha sekta ya michezo.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg.Khamis Mbeto Khamis, akizungumza na Vijana wa Kikundi cha Hamasa cha Jimbo la Chaani  katika ziara yake ya kuimarisha uhai wa CCM na kukagua Utekelezaji wa Ilani katika Jimbo hilo lililopo Wilaya ya Kaskazini ‘’A’’ .

NA: IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

CHAMA cha Mapinduzi Zanzibar, kimewataka viongozi wa majimbo nchini  kutekeleza miradi ya maendeleo itakayoacha alama za kudumu za maendeleo yatakayowanufaisha wananchi wote bila ya ubaguzi wa kidini,kisiasa na kikabila.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg.Khamis Mbeto Khamis,katika ziara ya kuimarisha uhai wa CCM katika jimbo la Chaani Wilaya ya Kaskazini ‘’A’’ Unguja.

Mbeto, alisema kuna baadhi ya wabunge,wawakili na madiwani nchini hawaonekani majimboni na wengine wanatoa ahadi za uongo kwa wananchi hali ambayo Chama Cha Mapinduzi hakiwezi kuendelea kuwavumilia.

Alisema viongozi hao ndio walioamua wenyewe kwa hiari yao kugombea nafasi za uongozi na wananchi wakawaamini na kuwapa ridhaa ya kuongoza hivyo ni lazima watekeleze majukumu yao.

“Huku majimbo kuna mambo mengi hayaendi sawa wapo baadhi ya viongozi wanatoa jezi na mipira ya michezo mbali mbali badala ya kufanya miradi ya maendeleo kwa wananchi wote na wengine hata majimboni hawaonekani kabisa mpaka wakati wa kukaribia uchaguzi na wengine ni mabingwa wa kutoa ahadi za uongo.

Rai yangu anzeni kujitathimini wenyewe kwani mafaili yenu yakiletwa kwetu basi hatutomuangalia mtu usoni kwani tumepewa dhamana kubwa ya kuongoza wananchi, rafiki yetu ni yule anayetekeleza Ilani ya CCM na kutatua kero na changamoto za wananchi.”, alisema Mbeto.

Amesema CCM, kitaendelea kuwafikishia wananchi wake maendeleo kwa wakati ikiwemo vituo vya afya ili wananchi wote wapate huduma za kiafya kwa wakati.

Amesema, kwa mujibu wa katiba ya chama cha mapinduzi, ukurasa  232 umetaja sekta ya afya utaimarisha hospitali na vituo vya afya katika wilaya na mikoa mbalimbali.

Amesema, chama cha CCM hakitaki kuona wananchi wake wanakwenda masafa ya mbali kufuata huduma za afya masafa makubwa na ndio serikali ikatilia mkazo uwepo wa hopsitali hizo.

Amesema kwa serikali imejenga hospitali za wilaya 12 zenye vifaa vya kisasa, kwa lengo la kuhakikisha afya za wananchi ziloimarika.

Amesema, serikali ya awamu ya nane imekuwa ikijenga hospitali za wilaya kila mikoa kwa lengo la kuona  wananchi wao wanaondokana na kufuata huduma za afya masafa makubwa.

Hata hivyo, aliahidi kuchangia gari ya mchanga na mifuko ya saruji ikiwa na lengo la kuona kituo hicho cha afya kinakamilika na wananchi wanatatua changamoto zilizokuwepo.

Amewasihi viongozi hao kufanya kazi kwa mujibu wa ilani ya CCM kwa vitendo ili kuona wananchi wake wanapata maendeleo kupitia viongozi wao.

Hata hivyo, aliwataka vijana wa hamasa kuacha tabia za kutumiwa katika mambo yasiyofaa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na badala yake wafanye kazi za kuhamasisha masuala mbalimbali ya Chama na Serikali zake.

Amezitaka Kamati za siasa za Mikoa na Wilaya kuanzisha utaratibu wa kufanya ziara za kutembelea majimbo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ili kubaini changamoto na mafanikio katika majimbo hayo.

Nae, Mwakilishi wa Jimbo la Chaani, Nadir Abdullatif, alisema, alitoa matofali 1000 na mifuko ya saruji 20  kwa lengo la kujengwa Kituo cha Afya cha Kisasa kitakachowahumia wananchi wa shehia ya Bandamaji kutokana na kutembea zaidi ya kilomita 5 kwa ajili ya kufuata huduma za afya.

Alisema, kituo hicho  kinajengwa kwa nguvu kazi za wananchi wenyewe walioamua kuchanga  fedha na kununua vitu mbalimbali ili kujenga kituo hicho ambapo kwa awamu ya kwanza walipeleka mawe.

Nadir, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya ujenzi,mawasiliano na uchukuzi Zanzibar, aliwashauri vijana hao wa hamasa kuanzisha vikundi vya ujasiriamali na awapatia mtaji wa zaidi ya shilingi milioni tano ili wajiajiri wenyewe.

Nae mkuu wa wilaya ya Kaskazini ‘’A’’, Sadifa Juma,  alisema ataendelea kupinga vikali tabia za baadhi ya wananchi kuhujumu fursa na miradi ya maendeleo ya wilaya hiyo.

Alisema katika kutafuta fursa ni vyema vijana wa maeneo husika kufanya kazi kwa kuzichangamkia fursa kwa kazi zilizokuwa hazina masharti mengi ili kuona vijana wanapata ajira.

Akizungumzia kundi la mahasa, na kusema lengo lake kuu ni kushajihisha na kuhamasisha masuala mbalimbali sambamba na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali kupitia kikundi hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here