Home BUSINESS BARRICK NORTH MARA, POLISI WATOA ELIMU YA USALAMA BARABARANI KWA WAENDESHA BODABODA...

BARRICK NORTH MARA, POLISI WATOA ELIMU YA USALAMA BARABARANI KWA WAENDESHA BODABODA TARIME

Askari wa usalama barabarani wakitoa elimu kwa waendesha bodaboda.
*
 
MGODI wa Dhahabu wa Barrick North Mara, umeshirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Tarime, kuwapatia madereva wa pikipiki za abiria (bodaboda) elimu ya usalama barabarani, ili kuepusha ajali katika maeneo yaliyo jirani na mgodi huo.
 
Elimu hiyo imetolewa wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, yaliyofanyika kiwilaya katika mji mdogo wa Nyamongo uliopo jirani na mgodi huo.
 
Mgodi huo umetumia nafasi hiyo pia kugawa msaada wa kofia ngumu 100 na jaketi maalumu 200 kwa baadhi ya waendesha bodaboda, huku Jeshi la Polisi likitumia vifaa mbalimbali kuwaelimisha sheria na alama za usalama barabarani.
Mkuu wa Kitengo cha Polisi wa Usalama Barabarani Wilaya ya Tarime, ASP Barnabas Irumba, amesema ajali nyingi zimekuwa zikisababishwa na madereva wa bodaboda wasio na elimu ya matumizi ya vyombo vya moto barabarani.
Awali, viongozi wa vijiji na kata jirani walikemea matumizi holela ya vyombo hivyo vya moto na kuwataka vijana waliojiajiri katika sekta hiyo kubadilika kwa kuhakikisha wanapata mafunzo stahiki na kuheshimu sheria za usalama barabarani.
 
Naye mwakilishi wa waendesha bodaboda waliohudhuria kilele hicho cha maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, aliyejitambulisha kwa jina la Msofe, ameushukuru mgodi wa Barrick North Mara, kwa msaada wa kofia ngumu na jaketi maalumu, na kwa upande mwingine Jeshi la Polisi kwa mafunzo ya sheria za barabarani, huku akiomba utaratibu uwe endelevu ili kujenga mahusiano baina yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here