Home LOCAL TANZANIA YAFUNGUA RASMI OFISI ZA UBALOZI NCHINI NAMIBIA

TANZANIA YAFUNGUA RASMI OFISI ZA UBALOZI NCHINI NAMIBIA

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imefungua rasmi Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Jijini Windhoek, Namibia.

Hafla ya ufunguzi wa ofisi hizo imefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na kulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania na Namibia wakiwemo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Mabalozi wa nchi za Afrika na viongozi wa jumuiya ya Watannzania wanaoishi nchini humo.

Akihutubia katika hafla ya ufunguzi, Mhe. Dkt. Tax ameishukuru Jamhuri ya Namibia hususan Wizara ya Mambo ya Nje kwa ushirikiano ilioutoa katika hatua zote za kuanzisha ofisi hizo pamoja na kushiriki tukio la kihistoria la ufunguzi ambalo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo.

Dkt. Tax pia alieleza kuwa kufuatia Tanzania kuwa mama wa lugha ya Kiswahili inaendelea na jitihada za makusudi za kuhakikisha Kiswahili kinatangazwa na kuenea kwa kasi kupitia Balozi zake, vyuo vya kimataifa na majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

“Wakati huu ambapo Serikali za Tanzania na Namibia zipo kwenye mazungumzo ya lugha ya Kiswahili kuwa sehemu ya lugha ya chaguo katika shule za Namibia, Ubalozi umefungua maktaba ndogo yenye vitabu na majarida ya Kiswahili kwa ajili ya watu wenye nia ya kujifunza kiswahili kuja kujisomea” alisema Dkt. Tax

Naye Mhe. Netumbo katika hotuba yake alieleza kuwa kwa sasa nchi hizo mbili zina makazi ya ubalozi katika miji mikuu ikiwa na lengo la kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo pamoja na watu wake.

Kadhalika, amempomgeza Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba kwa kuchagua jengo lenye ubora na la kisasa kwa ajili ya ofisi za ubalozi huo ambalo ni rafiki kwa mazingira.

“Tanzania ikiwa mpambanaji wa Bara la Afrika na Kusini mwa Afrika siku zote imekuwa pamoja nasi na hivyo sisi wanamibia tutakapokuja kujisomea na kufanya tafiti katika maktaba hii ya Kiswahili inayofunguliwa leo tutakuwa katika mazingira salama” alisema Mhe. Ndaitwah.

Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia ulianza utekelezaji wa majukumu yake ya kidiplomasia tarehe 20 Februari 2020 na kufanya Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba kuwa Balozi wa kwanza kuwaiwakilisha Tanzania katika nchi hiyo.

Hafla ya ufunguzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia imefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia unaofanyika Jijini Windhoek Namibia kuanzia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023 ambapo Mhe. Dkt. Tax ataongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo.

Wakati huo huo Waziri Tax alifanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Namibia ambao walijitambulisha kitaaluma ni Madaktari wa Binadamu.

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliwasihi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania wanapokuwa nje ya nchi pamoja na kuendelea na zoezi la kujiandikisha linalofanyika kwa watanzania wenye taaluma mbalimbali waliopo nje ya nchi ili waweze kutambulika na kuisaidia nchi yao katika taaluma hizo pale wanapohitajika.

Previous articleMICHUZI AIPONGEZA GGML KUNGUA FURSA KWA WANAWAKE, AAHIDI USHIRIKIANO 
Next articleTWCC, giZ WASHIRIKIANA KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI KUPITIA MRADI WA (WE4A)
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here